Mwenyekiti wa ALAT mkoa Kigoma Jackson Mateso akizungumza wakati wajumbe wa walipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya Kigoma
Nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kigoma ambayo wajumbe wa ALAT walitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wake
Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya Kigoma Tecla Lyuba (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa ALAT walipotembelea jengo la Utawala la halmashauri ya wilaya Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzanai (ALAT) mkoa Kigoma imekema tabia ya watendaji wa halmashauri za mkoa huo kuweka gharama za juu za bidhaa za manunuzi ya vifaa kwa ajili ya miradi ya ujenzi gharama ambazo hazizingatii gharama halisi iliyopo kwenye soko jambo linaloitia hsara serikali huku baadhi ya watendaji wakidaiwa wakijinufaisha na bei hizo.
Mwenyekiti wa ALAT mkoa Kigoma, Jackson Mateso alitoa kauli hiyo wakati wa ukaguzi wa mradi wa jengo la utawala la halmashauri ya wilaya Kigoma ambapo taarifa zilizotolewa Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya wilaya Kigoma, Exavery Ntambala zinaeleza mfuko mmoja wa sement kununuliwa kwa bei ya shilingi 24,000 hadi 25000 tofauti na bei ya soko ya Kigoma mjini ya shilingi 23,000 hadi 23,5000 kwenye maduka ya reja reja ya watu binafsi.
Aidha katika mradi huo wajumbe hao wa ALAT walibaini kuwepo kwa ununuzi wa bei ya juu wa tofali za block za kujengea ambapo taarifa inaonyesha kila tofali moja linanunuliwa kwa shilingi 2400 hadi 2500 wakati wanunuzi wengine wananunua kwa bei isiyozidi 2200.
Akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Kibondo,Habili Maseke alisema kuwa ni aibu kubwa kuona wasimamizi wa miradi kwenye halmashauri wakiweka viwango vya juu vya gharama za ujenzi kuliko bei ya soko na hii yote inadhihirisha ubadhirifu wa wahandisi na maafisa manunuzi wa halmashauri jambo linalofanya utekelezaji wa miradi kuwa mgumu.
Maseke alisema kuwa miradi mingi inatekelezwa kwa kutumia mafundi kutoka eneo husika (Force Account) badala ya wakandarasi lakini cha kushangaza miradi inayotumia utaratibu huo inakuwa na gharama za juu kuliko zonazotumia wakandarasi.
Akieleza kuhusu tuhuma hizo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Exavery Ntambala alisema kuwa kuwepo kwa gharama za juu za sementi na tofali kunatokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo kuanzi mwezi Oktoba mwaka jana kutokana na mvua kubwa hivyo barabara kutopitika kwa urahisi.
Katika ziara hiyo wajumbe hao wa ALAT walitembelea ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kukiwa na nyumba mbili za watumishi kwa wakati mmoja zenye thamani ya shilingi milioni 270 ambapo kwenye nyumba ya Mkurugenzi walishuhudia kuwepo kwa jakuzi la kuogea chooni lenye thamani ya shilingi milioni 6.5.
Mwisho.
0 Comments