Na Thobias Mwanakatwe, DODOMA
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Inades Formation Tanzania (IFTz) linalojishughulisha na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na ustawi wa kijamii limeiomba serikali kuingiza mnyama punda katika mtaala wa masomo ya ustawi wa wanyama ambayo itasaidia wataalamu wanaomaliza vyuo vya afya na tiba ya mifugo kuwa na uwezo wa kumhudumia mnyama huo.
Daktari wa Afya na Tiba ya Wanyama wa shirika hilo,Dk.Charles Bukula, akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanahabari juzi alisema mtaala wa Tanzania haujamzungumzia punda kama ilivyo kwa wanyama wengine kama farasi hali inayosababisha akose haki za msingi ikiwemo za matibabu.
Alisema pia serikali pamoja na wadau wa ustawi wa wanyama (animal welfare organizations) izipitie upya kanuni za ustawi wa nyama ili punda kujumuishwa kama mnyama anyaeomekana kutoweka (endangered species).
"Ifike wakati jamii imthamini punda kama inavyothamini wanyama wengine kwa kumpatia matibabu,lishe bora na kutosababishiwa maumivu yasiyo ya lazima,mfano kupigwa hovyo wakiamini kuwa punda haumii," alisema.
Dk. Bukula alisema katika kuendelea kumdhamini punda, Serikali itenge mwezi Mei kuadhimisha siku ya punda duniani ambayo itakuwa inaadhimishwa kila mwaka kama wanavyoadhimisha siku ya ugonjwa wa kichaa duniani kwa lengo kutoa hamasa kubwa kwa punda kupewa thamani kama wanyama wengine.
Aliongeza kuwa Shirika la IFTz linatambua kuwa kama punda akistawi jamii itamtumia kwa muda muda mrefu na kumpatia kipato pale anapotumika katika shughuli za usafirshaji mizigo.
Alisema punda kama ilivyo kwa wanayama wengine anazo haki ambazo ni pamoja na haki ya kutopata njaa, kiu au udhoofu wa mwili, haki ya kupewa chakula bora na maji ya kunywa,haki ya kuwa huru dhidi ya hofu na msongo wa mawazo na haki ya kutosumbuliwa kifikra
Nyingine ni haki ya kuwa huru dhidi ya usumbufu wa mwili wake, haki ya kuwa huru dhidi ya maumivu, majeraha na magonjwa na pia ana haki ya kukingwa dhidi ya maradhi, majeraha au maumivu.
Shirika la IFTz linaendesha mradi wa kuboresha maisha ya jamii kupitia ustawi wa mnyama punda kwa ufadhili wa Shirika la Brooke East Africa mradi ambao unaendeshwa katika mikoa ya Dodoma,Iringa na Singida.
Malengo mahsusi ya mradi huo ni kubadilisha na kuboresha ustawi wa punda wanaofanyakazi katika jamii, kuwasaidia katika kustawi na kuendeleza ustahimilivu zaidi,kuongeza vishawishi ili kusaidia kuingizwa kwa mahitaji ya punda katka Sera na desturi ikiwa ni pamoja na maandalizi ya maafa na dharura.
Malengo nengine ni kutengeneza mifumo dhabiti ya afya ya wanyama inayokidhi mahitaji ya haraka na ya baadaye kwa punda wanaofanyakazi.
0 Comments