Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Pangani.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Tanga Rajab Abdurahman ameitaka jamii kutowafumbia macho wanaume wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kusababisha kukatiza ndoto zao za kielimu kwa kuwapa mimba
Rai hiyo ameitoa wakati akiongea na wananchi wa kata ya Masaika wilayani Pangani baada ya kukagua maendeleo ya shule ya Msingi Masaika na kukutana na changamoto za utoro na mimba kwenye shule hiyo.
Alisema kuwa ni vema jamii iweze kuwa mstari wa mbele wa kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu na iwapo watabainika kuwa wanaume wasio na maadili wabawarubuni wachukuliwe hatua.
"Tuwasaidie watoto wa kike ambao walirubuniwa na wanaume mafataki na kuwapa mimba kwa kuhakikisha sheria zinachukuwa mkondo wake badala ya kumalizana kienyeji"alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa changamoto ya mimba kwa wanafunzi zisipo dhibitiwa mapema zinakwenda kudumaza dhamira nzuri ya Rais Samia ya kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma huku wengine wanaishia njiani kutokana na kupata mimba wakiwa shuleni.
"Hakikisheni wazazi na walezi hizo kesi zinafikishwa kwenye vyombo vya sheria na jamii msimamie haki iweze kupatikana Kwa mtendewa Ili iwe fundisho kwa wanaume mafataki "alisema Mwenyekiti Rajab.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Masaika Sophia Kihebu alisema kuwa kwa mwaka Jana shule hiyo ilipata changamoto ya wanafunzi wake wawili wa darasa la sita kupata ujauzito na hivyo kukatiza masomo yao.
Aidha alisema kuwa changamoto ya mimba za utotoni sambamba na utoro vinachangiwa kwa kiasi kikubwa na umbali wa shule hiyo ambapo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 8.
"Ufaulu wa shule yetu Kwa mwaka 2022 ni asilimia 87 ambapo unasababisha na utoro pamoja na mimba za utotoni kutokana na umbali wa makazi ya wananchi kuja kwenye eneo la shule"alisema Mwalimu Kihebu.
Hata hivyo Kihebu alisema kuwa shule hiyo inachangamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo sambamba na nyumba za walimu.
0 Comments