Header Ads Widget

TUSITELEKEZE CHIMBUKO LETU (IJUKA OMUKA) "GALA DINNER" ILIYOFANYIKA MJINI BUKOBA - KAGERA


Jioni ya tarehe 22 Desemba, 2023 katika ukumbi mpya ambao ni kitegauchumi cha Kagera Cooperative Union (KCU); Mkuu wa mkoa wa Kagera, Hajja Fatuma Mwasa, chini ya uratibu wa ofisi yake, aliandaa tukio adhimu la hafla ya chakula cha jioni. Hafla hiyo ilipewa jina la "Ijuka Omuka Gala Dinner", kwa vile tukio lilibeba ujumbe maalumu wa "wanaKagera sote tuguswe na tukumbuke chimbuko letu, tujenge Kagera yetu".


Hakika, tukio hilo adhimu haliwezi kuachwa lipite bila kufanyiwa andiko maalumu (documentary)

kwa minajili ya kumbukumbu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo!


Waalikwa walikuwa anuwai; wakiwa ni pamoja na wabunge wanaotoka katika mkoa wa Kagera, viongozi wa serikali ya mkoa na taifa. Mathalan, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Ujenzi, Mh. Innocent Bashungwa, bila kumsahau mbunge mwenyeji, Mh. Stephen Byabato, ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Waalikwa wengine walikuwa wasomi, viongozi wa vyama vya kisiasa, viongozi wa kidini, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wavuvi na wenyeji wengine ambao hawamo katika makundi ambayo yametajwa, wakitoka katika wilaya zote zinazounda mkoa.


Hafla hiyo ilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa kwa hotuba maridhawa iliyosheheni matumaini. Aidha, alibainisha fursa lukuki zilizomo katika mkoa wa Kagera na kuhamasisha wawekezaji (investors) wa ndani na nje kuchangamkia fursa tajwa. Isitoshe, alielezea tukio lililochochewa na wapenda maendeleo lililohusu ujenzi wa uzio wa bweni la wanafunzi wasichana wa sekondari ya Bukoba, mjini Bukoba. Uzio huo ulijengwa na kukamilika kwa juhudi zilizotokana na uungwaji mkono wa uhamasishaji wake. 


Wakati wa hafla hiyo, waalikwa walipokea ombi murua kutoka kwa Mkuu wa Mkoa lililohusu ujenzi wa uzio mwingine kwenye sekondari ya Omumwani, katika kiunga kimojawapo cha mji wa Bukoba. Mwitiko ulikuwa wa kuridhisha. Michango ya pesa taslimu pamoja na ahadi za michango ya pesa na vifaa vya ujenzi vilivyotokana na harambee ya papo kwa papo, jumla yake ilikadiriwa kuwa shilingi milioni sabini (70).  Mfanyabiashara kutoka wilaya ya Karagwe, Ndg. Kachebonaho, alitia fora kwa kuchangia milioni kumi na saba (17).


Kadhalika, Profesa Rutinwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika Kitivo cha Sheria, kampasi kuu iliyopo Dar es Salaam, aliwasilisha mada kuhusu elimu, na kutoa taarifa bainifu juu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanza kujengwa katika kata ya Karabagaine, Bukoba Vijijini. Pia, mpango wa ujenzi wa chuo kikuu kingine cha uvuvi na uandaaji wa vizimba vya samaki maeneo ya Bugabo, karibu na ziwa Victoria, vilevile Bukoba Vijijini.


Profesa Anna Tibaijuka alitoa mada iliyoakisi mojawapo ya mazao  makuu ya chakula mkoani Kagera, yaani ndizi, na zao la biashara, kahawa. Alifafanua kwamba kudorora kwa mashamba (ebibanja) ni matokeo ya ardhi kutumika kiujima kwa muda mrefu, hivyo rutuba yake kupungua. Kati ya athari za kudorora huko, ni kushamiri kwa utapiamlo na udumavu wa watoto. Alihitimisha kwa kutoa suluhisho ya kuwa kuna ulazima wa kurejea kwenye ufugaji, hasa wa ng'ombe, ili kuweza kupata mbolea "samadi" kwa lengo la kurudisha tija ya awali ya mashamba hayo.


Mgeni rasmi, Waziri wa Ujenzi, alihimiza wasomi kutoka mkoa wa Kagera kufanya utafiti wa kina kwa nini mkoa huu unaorodheshwa kwenye mikoa yenye umaskini uliokithiri kitaifa. Alidai kwamba pengine hali hii haina uhalisia. Vivyo hivyo, aliwasihi wanaKagera kuwa na mshikamano na kuacha malumbano ambayo kwa kiasi kikubwa hayana tija. Umoja uwe chachu  na nguzo kwa wanaKagera kwa mustakabali wa mkoa. Kwa umoja huo, bila kubaguana kwa misingi ya dini, rangi, nasaba, maeneo,  wala vyama vya kisiasa, kusudio mujarabu liwe kujenga Kagera mpya.


Zaidi ya hayo, mgeni rasmi alitoa tuzo kadhaa kwa wale waliochagiza maendeleo ya mkoa katika miaka ya karibuni. Kwa mfano,  Ndugu Justin Kimodoi anayeishi nchini Marekani, alipewa zawadi kwa niaba ya wenzake, wapenzi wa maendeleo, wanaoishi ughaibuni (diaspora). Ndugu Kakiziba, msanifu (architect), naye alipewa zawadi kwa kujitolea kusanifu uzio wa bweni la wanafunzi wasichana wa sekondari ya Bukoba na kusimamia ujenzi wake. Naye Ndugu William Ruta (aka - will i am) alizawadiwa kwa kuzingatia uhamasishaji wake madhubuti katika  kutangaza vivutio vya utalii mkoani Kagera. 


Tuzo pekee ya heshima ilikabidhiwa kwa *Hajjat Fatuma Mwasa*,  Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Huyu mama, tofauti na wakuu wa mkoa wa Kagera waliomtangulia, ana maono ya kipekee kwa ustawi wa mkoa. Kwa hiyo, alimiminiwa sifa kedekede  kwa ndoto ya kuandaa kusanyiko hilo lililowakutanisha wanaKagera kwenye chimbuko lao (nyumbani) kutokana na wito "*Ijuka omuka*"! 


Kwa uhakika, ni tukio adhimu kwa masilahi ya "*Kagera tuitakayo*". Ni tukio linalopaswa kuwa na muendelezo, kuwa linajirudia. Mwaka huu (2024) liandaliwe na kutangazwa mapema ndani na nje ya nchi. 


Hata hivyo, yafuatayo ni maoni na ushauri wangu.

Wigo wa mialiko, endapo mialiko ni lazima,  upanuliwe. Pia, tarehe au siku itakayopangwa,  iwe rafiki kwa kiasi kikubwa kwa wale watakaowiwa kuhudhuria. Mathalan, siku au tarehe baada ya sikukuu ya Krismasi na kabla ya mkesha wa mwaka mpya inaweza kuwa mwafaka. Tarehe iliyopangwa mwaka jana (2023) haikuwa rafiki, kwani wengine siku hiyo ndipo walikuwa safarini kuelekea Kagera.

Mwisho, pengine tukio hili likifanyika mara mbili, tatu, na kupata uzoefu, kuna haja ya kuanza mzunguko. Mwaka fulani   likafanyika Ngara, mwingine Kyerwa, mwingine Biharamulo, nk.


Na;- Nazalary .A. Kiobya, shamteabas@gmail.com. tel 0759 336318

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI