Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameonyesha furaha yake kubwa baada ya kutimiza ahadi na ndoto yake ya muda mrefu ya kujenga jengo la kupumzikia ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo, Mavunde alisema kuwa dhamira hiyo aliiweka tangu akiwa mgombea ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010, ingawa hakufanikiwa wakati huo.
Alieleza kuwa alitamani sana kupata nafasi ya uongozi katika eneo alilozaliwa ili aweze kuchangia maendeleo na kusaidia wananchi kwa dhati
Mavunde alisema kuwa alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015 aliahidi kwa wanachi kuwa mtumishi wa watu badala ya kuwa kiongozi wa kawaida.
Alianza kushughulikia changamoto nyingi zilizokuwa zikikumba sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na uchelewaji wa huduma na malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji wa baadhi ya watumishi.
Mwaka 2017 alianzisha mfumo wa kidijitali kuhakikisha kuwa watumishi wanafika kazini kwa wakati na kuwatendea wagonjwa kwa heshima. Alieleza kuwa alifunga kamera na maikrofoni katika eneo la huduma za wagonjwa wa nje ili kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora.
Mbunge huyo alikumbuka tukio la siku moja alipofika usiku hospitalini akiwa ameambatana na mgonjwa na kukuta wananchi wengi wamelala nje ya geti wakichanganyika bila kujali jinsia.
Alisema hali hiyo ilimuumiza sana na kumfanya aazimie kujenga jengo la kupumzikia ili kuwasaidia wananchi hao. Jengo hilo lina mabenchi 24 ya kukalia, televisheni kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu na uzio kwa ajili ya usalama.
0 Comments