NA HADIJA OMARY LINDI
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Lindi imefanikiwa kudhibiti kiasi cha shilingi milioni 6.8 kutoka kwa wafanyabiashara ambao pia ni wazabuni katika miradi ya ya ujenzi Wilayani Nachingwea kwa kutoa lisiti za mikono kwa kamati za ujenzi badala za EFD kama miongozo ya Serikali inavyotaka
Hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi mha. Abnery Mganga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kueleza shughuli za utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha January hadi Disemba 2023.
Mha. Mganga amesema katika kipindi hicho Taasisi hiyo iliweza kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya mashine za EFD kwa wazabuni watoa huduma za vifaa vya ujenzi katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa Wilayani humo ambapo amesema kuwa endapo wasingefanya ufuatiliaji huo ni wazi kwamba serikali ingepata hasara.
Hata hivyo Mhandisi Mganga alisema kuwa katika kipindi hicho pia juhudi za mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mkoa huo zimewezesha kuimarika kwa utoaji wa huduma mbalimbali, usimamizi wa fedha za Umma, kuongezeka nidhamu , uadilifu na uwajibikaji katika utumishi wa Umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za Afya na Elimu.
Mganga pia alisema Taasisi hiyo imejipanga katika robo ya tatu ya mwaka inayoanzia januari - march 2024 kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kudhibiti vitendo vya Rushwa kwa kufanya ufuatiliaji wa kina kuhusiana na manunuzi pamoja na malipo mbalimbali katika miradi ya maendeleo pamoja na mapato ya serikali.
0 Comments