Header Ads Widget

TANROAD KILIMANJARO YAREJESHA MAWASILIANO YA BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA MVUA.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME. 


WAKALA wa barabara nchini (Tanroad) mkoa wa Kilimanjaro imefanikiwa kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara zilizokuwa zimeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwa asilimia 90.


Hayo yamebainishwa na Meneja wa Tanroad mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi  Motta Kyando katika ziara ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kutembelea barabara kuu ya Same - Dar es salaam katika eneo la Hedaru na Makanya wilayani Same yaliyoathiriwa na mvua. 



Mhandisi Motta alisema kuwa, kutoka na mvua zinazoendelea kunyesha zipo barabara ambazo zinasimamiwa na Tanroad ziliathirika na kupelekea kukatisha mawasiliano kwa muda lakini kwa sasa hali imerejea ambapo Wakandarasi wapo saiti kumalizia shughuli ndogondogo. 


Alisema kuwa, katika eneo la Hedaru wamebaini daraja lililopo ni dogo hali inayopelekea kuziba na kuruhusu maji kupita juu ya barabara ambapo kwa sasa wamefanya kazi ya kufungua daraja hilo ili maji yaweze kupita katika njia yake. 


"Maeneo haya ni ya milimani hivyo mvua zilinyesha huko na kupelekea maji kushuka mengi yakiwa na magogo na mawe makubwa pamoja na udongo na kupelekea mdomo wa daraja kuziba na kuruhusu maji kupita juu ya barabara na kukatisha mawasiliano kwa muda" Alisema Mhandisi Motta. 



Na kuongeza kuwa "tumekuja kubaini maji yanayopita eneo hili ni mengi ikilinganishwa na daraja hili hivyo msimu wa mvua ukipita tutaongeza daraja hili ili kuhimili maji haya na kuepuka matatizo haya".


Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliipongeza Tanroad kwa jinsi ambavyo wamechukua hatua za haraka kuhakikisha mawasiliano yanarejea kwa haraka. 


Babu alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujenga kwenye njia za maji kwani yanapokosa mwelekeo huingia katika makazi ya watu na kuharibu mali.



"Hapa Hedaru mvua zimepelekea vifo vya ndugu zetu watatu haya ni madhara makubwa hivyo niwaombe wananchi epukeni kujenga katika njia za maji na pia mnapoona mvua zinanyesha kubwa msijaribu kuvuka kwenye mito kwani mnaweza kusombwa na maji" Alisema Babu. 

Mwisho.. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI