WANANCHI wa Kisiwa cha Songosongo Wilayani Kilwa wahofia kuendelea kupata ama kuenezwa kwa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi katika maeneo yao kwa kile kilichodaiwa kuingia kwa kundi kubwa la wasichana kwa nia ya kufanya biashara za kingono maarufu kama kijoti
Hayo yameelezwa na Mwalimu Haji ibrahim alipokuwa anasoma risala ya kikundi cha maendeleo ya jamii Songosongo (KIMAJASO) wakati wa tamasha la ukimwi lililolenga kutoa Elimu ya Ukimwi , Lishe pamoja na kupima Afya lililoandaliwa na Kikundi hicho kwa kuwezeshwa na kampuni ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia (SONGAS).
Amesema kutokana na uwepo wa makampuni mengi kisiwani hapo yanayofanya shughuli ya uchakataji wa gesi wasichana wengi wamekuwa wakivutika kuingia kisiwani na kufanya biashara hiyo ya ngono.
" eneo letu hili ni moja ya maeneo ambayo watu huwa wanaingia na kutoka hivyo tunazo athari zingine ambazo ni muingiliano huu wa watu imefikia hatua tunapokea magonjwa kutoka kwa watu ambao wanatoka tusipopajua wanakuja hapa"
"Mfano tunakundi la watu fulani linaitwa vijoti maarufu kama Dada poa wakiingia hapa wanafanya shughuli ya kuiuza miili yao kwa bei rahisi sana kwa hivyo mtu akiwa na Elfu moja Elfu mbili anaenda huko bila kujua alikotoka ana historia gani mwisho wa siku tunaachiana magonjwa ambayo yanaathiri Afya za wanajamii hii ya Songosongo "
Kwa upande wake Jafari Kasimu Muelemishaji Rika kutoka katika kikundi hicho cha KIMAJASO Amesema Jamii za watu wanaoishi katika visiwa hawana tofauti na watu wanaochezea viwembe ama vitu vyenye ncha kali kutokana na mazingira ya muingiliano wa watu katika Eneo husika.
" kwa kuwa kuna muingiliano unaotokana na shughuli zinazofanywa na makampuni yaliyokuwepo katika kisiwa hicho kama vile Songas, Pan Africa Energy na makampuni mengine mengi yajayo na yatokayo , wapo wanaofanya kazi ndani ya wiki moja mbili wakaondoka, wapo tunaokaa nao miezi mitatu kwa hakika lazima wawe na matamanio ya kuweza kuwapata akina Dada"
Nae maneno Abdalah mwananchi wa kata hiyo ya Songosongo amesema matamasha ya namna hiyo yanapofanyika yanatoa fursa ya wananchi kujikumbusha maswala mbalimbali yanayochangia kuenezwa kwa ugonjwa huo wa ukimwi pamoja na namna ya kujilinda .
"Elimu juu ya ugonjwa wa Ukimwi bado inahitajika hivyo tunayaomba makampuni yanayotekeleza miradi katika kisiwa chetu waendelee kutushika mkono ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi" alisema maneno
0 Comments