Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Hand in Hand Eastern Africa Tanzania limezindua tawi lake katika Mkoa wa Singida ambapo malengo yake ni kuwasaidia wajasiriamali zaidi ya 16,000 wa mkoa huu ili waweze kuunda biashara 11,200 zitakazotengeneza ajira 17,388 na hivyo kuwainua kimapato na kukuza mabadiliko ya kimfumo ya usawa wa kijinsia.
Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo (CEO), Albert Wambugu, akizungumza jana (Disemba 5, 2023) wakati wa uzinduzi wa ofisi za shirika hilo, alisema tawi la Singida ni la tano ambapo matawi mengine yapo Arusha,Moshi,Dodoma na Babati mkoani Manyara.
Alisema lengo la shirika hilo ni kupambana na umaskini kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye vipato vidogo chini ya Dola mbili za Kimarekani kwa siku.
Wambugu aliishukru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kibali kwa Shirika la Hand in Hand Eastern Africa Tanzania kuweza kufanya shughuli zake katika Mkoa wa Singida na mikoa mingine hapa nchini.
Alisema matarajio ya shirika ni kuona biashara zinainuka na mtu akianza biashara yake inadumu kwa zaidi ya miaka miwili bila kuteteleka na pia pato linaongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 hususani kwa wanawake.
Naye Meneja wa Nchi wa shirika hilo (Country Manager), Jane Sabuni, alisema shirika hilo tangu limeanza kufanya kazi zake hapa nchini 2018 limeweza kuwawezesha wajasiriamali wasiopungua 37,000,kuanzisha biashara zisizopungua 38,000 na hivyo kutengeneza ajira zaidi ya 39,000.
Sabuni alisema kwa Mkoa wa Singida ambako miradi itatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya ya Ikungi,Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Manispaa ya Singida,matarajio ya shirika ni kuwafikia wakulima wa zao la alizeti,wafugaji wa kuku na nyuki ili kuwaongezea kipato na hivyo kujikwamua na umaskini kupitia ajira na biashara endelevu.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika hilo tawi la Singida, Glory Temu, alisema miradi itakayotekelezwa na shirika hilo kwa Mkoa wa Sibgida ni mradi wa Inua ambao utasaidia wajasiriamali 6,250 asilimia 80 wakiwa ni wanawake na asilimia 20 wanaume ambao wataunda biashara 4,375 na kutengeneza ajira 5,688.
Alisema mradi huo utachukua miezi 41 kuutekeleza utatumia hatua nne za shirika ambazo ni uhamasishaji wa watu kujiunga kwenye vikundi,mafunzo ya biashara,kuwaunganisha wanavikundi kupata mikopo katika taasisi za kifedha na kuwaunganisha wanakikundi na masoko.
Temu alisema matokeo yanayotarajiwa katika mradi huu ni kuongeza faida na uimara wa kibiashara kwa wanachama,kuinua kipato,kurasimisha shughuli za kuongeza thamani katika mradi na kusaidia vikundi kuunda asasi za kijamii (CBOs) na faida kutoka viwango vya kiuchumi.
Aliongeza kuwa mradi mwingine utakaotekelezwa ni New Gunvor ambao lengo lake ni kusaidia wajasiriamali 9,750 asilimia 80 wakiwa ni wanawake ambao watatengeneza biashara 6,825 na ajira 11,700.
Alisema mradi huo umepangwa kuchukua miezi 16 ambao pamoja na mambo mengine utasaidia kuondoa vikwazo vya kijinsia vinavyozuia uwezeshaji wanawake,mafunzo ya ziada ya jinsia ambayo yatashughulikia sheria zenye madhara ili kutetea usawa na ushirikishwaji wa wanawake.
Naye Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Raslimali Watu, Stephen Pancras,ambaye alikuwa mgeni rasmi kumwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Singida,Dk Fatuma Mganga,akisema kwa kuwa sera ya serikali ni kuwatumikia wananchi hivyo ujio wa shirika la Hand in Hand Eastern Africa Tanzania ni muhimu sana ili kusaidiana na serikali kuhudumia wananchi.
"Niwapongeze viongozi wa juu makao makuu ya Hand in Hand Eastern Africa Tanzania kwa kukubali kutoa fedha kuzileta Tanzania ili kusaidia Watanzania pale ambapo serikali inakuwa haijafanya," alisema.
Pancras alisema kwa kuwa shirika hilo limekubali kufanya kazi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lihakikishe linafuata na kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza yake mkoani hapa na nchini kwa ujumla.
"Watumishi wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania niwaase hakikisheni mnapohudumia wananchi msiwakwaze,mzingatie sheria na tamadanuni ili msionekane ni changamoto katika maeneo mtakapokuwa mnatoa huduma,suala la maadili lizingatiwe taaluma mlizosomea ziwaongoze katika uchapa kazi wenu," alisema Pancras.
Aidha, Pancras aliwaasa watumishi wa umma kutokuwa kikwazo cha kukwamisha shirika hilo lisiweze kutekeleza majukumu yake badala yake wawaongoze ili mipango waliyoweka iweze kufikiwa kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi.
0 Comments