Header Ads Widget

IAA KUPAA KIMATAIFA CAMPUS YA KWANZA NJE YA NCHI KUANZA JUBA, SILINDE ASISITIZA TAFITI WALIZOFANYA WAHITIMU ZIKATUMIKE KUTATUA CHANGAMOTO KATIKA JAMII.

NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA

Naibu waziri wa Kilimo David Silinde amewataka wahimu waliohitimu kozi mbalimbali katika chuo cha Uhasibu Arusha(IAA) kutokufungia matokeo ya tafiti walizozifanya badala watumie  matokeo hayo katika kutatua changamoto zinazozikabili jamii zinazowazunguka.


Silinde aliyasema hayo wakati akihutubia katika maafali ya 25 ya chuo cha uhasibu Arusha kwa niaba ya waziri wa Fedha Dkt Mwingulu Nchemba ambapo alisema kuwa kila muhitimu akitumia vizuri matokeo ya utafiti alioufanya na kuushirikisha katika jamii husika ya mahali alipo utakuwa umetatua baadhi ya changamoto.

“Msifungie matokeo ya tafiti zenu baada ya kuhitimu, yatumieni, shirikisheni jamii ili yaweze kuwa chachu katika kuleta mabadiko chanya, kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi na utendaji kazi wa kila siku, usimamizi wa taasisi na mashirika, uboreshaji wa sera pamoja na mipango na mikakati kwa maslahi mapana ya taifa letu,” Alisema Silinde.


Aidha aliwahimiza kuendelea kujifunza, kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuwa raia wema kwa jamii na taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kutafakari namna watakavyotumia elimu waliyoipata kupambana na umasikini na kuleta maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.


“Serikali, wazazi, walezi na wafadhili wenu tuna matumaini makubwa nanyi kwamba uwekezaji tuliofanya kwenye elimu yenu haikuwa bure bali matokeo ya tija ya elimu mliyoipata yataonekana dhahiri kwenye mchango wa kila mmoja katika maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,Alieleza.

Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Profesa Eliamani Sedoyeka alisema kuwa wana kozi 71 ambapo kati ya kozi hizo 16 ni ngazi za shahada, 17 ni stashada, 24 astashahada na kwa upande wa uzamiri wana kozi 14 ambapo pia wanaendelea na zoezi za uhuishaji wa mitaala ili kuhakikisha chuo kinatoa kozi ambazo zinaendana uhalisia na mahitaji ya soko.


“Sisi Misingi yetu ni weledi na umahiri na kwa niaba ya serikali tunaendelea kuishi katika hiyo misingi yetu  kwa maana ya  profesionalism and excellence ikiwa ni pamoja na kuendelea kutengeneza mitaala mbalimbali, kufanya tafiti ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha tunaendelea kuwa kinara,” Alisema Prof Sedoyeka.


Alifananua kuwa Mpango mkakati wa chuo hicho kwa miaka mitano 2022/2027 ni kuendelea kupanua wigo ndani na nje ya nchi na mpaka sasa wana Campus 4 ikiwemo ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma na Babati na wanatarajia kuanzisha Songea na ambapo tayari wana eneo serikali imeshawatengea bajeti ya takribani shilingi bilioni 22 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.


“ Kwa Dodoma kwa kutumia fedha zetu za ndani tumeshaanza kujenga jengo ambalo litaweza kukalisha wananfunzi 4500 kwa mara moja lakini pia kimataifa  tumefanya mikakati mbalimbali ikiwemo ziara Sudan ya Kusini na tupo tayari kuanzisha campus ya kwanza nje ya nchi Juba katika mwaka ujao wa masomo,” Alisema Prof Sedoyeka.


Alifafanua kuwa kutokana na uhalisia Campus za Ruvuma na Babati zimejikita katika uchumi wa kati ikiwemo shughuli za kilimo, ufugaji, usindikaji, utalii na kuendelea kutoka na ndio ukweli na uhalisia wa maeneo hayo ambapo pia wameanzisha ushirikiano na chuo cha Polisi Moshi kwa kuanza kutoa kozi mbalimbali zinazolenga ulinzi na usalama.

 

Naye makamu mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo CPA Joseph Mwigune alieleza kuwa  katika mahafali hayo wamehitimu jumla ya wanafunzi 5387 ambapo katika ngazi ya shahada ya uzamili wana wahitimu 1139, ngazi ya shahada 1027,ngazi ya Stashahada 1260 na ngazi ya Astashahada 2061.


“Kwa kutambua mchango wa vyuo vya elimu ya juu katika kutoa elimu bora , kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalamu, kuendeleza rasilimali watu, kujenga na kuimarisha utamaduni wa kujifunza, kuimarisha ujuzi na ubora wa wafanyakazi, chuo kimeendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali ili jamii na taifa liendelee kunufaika kupitia uwepo wake,” Alisema CPA Mwigune.


“Chuo kimeendelea kutoa elimu kwa kupitia wataalamu mahiri, miundombinu bora na rafiki inayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na mitaala bora inayowaandaa wanafunzi mahiri wenye ujuzi na maarifa yanayohitajika wakati wa sasa na ujao,” Alieleza.


Hata hivyo mmoja wa wahitimu  Shedrack Sebastian rais mstaafu wa serikali ya wanafunzi 2023 alisema kuwa walifika katika chuo hicho wakiwa hawana kitu lakini wametoka wakiwa vijana mahiri na wenye uwezo,watakaoenda kuisaidia  jamii na taifa ambapo wametoa shukrani kwa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kuipa kipaumbele suala la elimu kwani elimu ni ufunguo wa maisha na wameona mabadiliko mengi katika chuo chao ikiwemo ya Miunfombinu.


“Vijana wenzangu twendeni tukawe sehemu ya faraja kwa wazazi wetu na taifa kwa ujumla kwani taifa lenye wasomi wanaoshikamana huleta chachu ya mabadiliko kiuchumi, kisiasa na maendeleo kwa ujumla,tusiwe mzigo kwa taifa lakini pia tuache kukesha tukiisema serikali badala yake twende tukaishauri na kufanya tafiti mbalimbali zenye tija na kutumia njia bora kutoa maoni ili taifa letu liweze kusonga mbele,”Alisema Shedrack.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI