Na Matukio Daima Media ,Mbeya
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya Mhashamu ,Gervas Nyaisonga amesema wamesikitishwa na maafa makubwa ya maporomoko ya udongo yaliyotokea mlima Hanang Mkoa wa Manyara ambayo yameathiri mji mdogo wa Katesh na kusababisha vifo vya watu 65 na kaya zaidi ya 1,150 kuathiriwa vibaya,
Katika maafa hayo yamepelekea watu 5,600 kuathirika na mafuriko huku wengi wao walionusurika wakiwa wamehifadhiwa kwenye majengo ya Kanisa,Shule na kwa watu wengine wenye mapenzi mema .
Mhashamu Baba Askofu Nyaisonga ametoa kauli hiyo leo Jumatano ,Desemba 6,2023 kwa niaba ya baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Jimbo Kuu la Mbeya kuhusiana na maafa hayo makubwa kwa taifa.
“Hili ni tukio baya la maafa makubwa ambayo yanasikitisha tunatoa pole kwa wananchi wote wa Hanang na Mkoa mzima wa Manyara ,watanzania wote pia kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na tunakiri maafa haya yana mguso wa kimazingira yasiyo epukika kwa udharura wa papo kwa papo “amesema.
Ameongeza kuwa “Tunakiri kuwa maafa haya yamesababisha vifo vingi na upotevu wa mali pamoja na uharibifu wa miundo mbinu na kupelekea usumbufu mkubwa wa watu , kikubwa tuishukuru serikali kwa hatua za dharura walizochukua , wanajeshi askari wetu, na watu wote waliojituma kushughulikia uokoaji wa haraka kwa watu walioathirika”amesema Mhashamu Baba Askofu Nyaisonga.
Aidha Askofu Nyaisonga amewatia moyo walioathiriwa na maafa hayo na kuwashukuru wale wote waliotoa msaada huku akiwataka watanzania wote kutokata tamaa kwa kuwa wakalimu kwa wananchi waliokutwa na maafa hayo makubwa waendelee kumwamini Mungu kuwa anawapenda na kuwapa ujasiri pamoja na kuendelea kuwaombea majeruhi wote.
Akizungumzia kuhusu msaada kwa waathirika Askofu Nyaisonga amesema kuwa tayari wameanza kuratibu utaratibu wa kupeleka msaada kupitia kitengo cha Caritas kinachoshughulikia maafa ikiwepo Dawa , vyakula , mavazi na mbegu za mashamba tayari waraka umesaniwa kwa ajili ya kukabidhi vitu hivyo .
“Huo sio mwisho wanaendelea kuwasiliana na wahisani wao ndani na nje ya nchi pamoja na washirika ili kuendelea kutoa misaada.
Aidha amesema kuwa kwa upande wa baraza la maaskofu wanaendelea kuratibu kupitia kitengo cha maafa cha CARITAS na kuhamisha kwenyemajimbo kuchangia misaada hiyo .
Mwisho.
0 Comments