Katika kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi wa mwaka 2021 – 2026 mashirika 6 yanayojihusisha na utunzaji wa mazingira na tabia nchi ya jijini Mwanza yameanza kampeni ya kubadilisha tabia za wananchi katika utunzaji wa mazingira kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari mwanaharakati wa mazingira na mjumbe wa mtandao wa kijinsia na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania Sophia Donald amesema suala la mabadiliko ya Tabia Nchi linagusa watu wa jinsia zote hivyo mpango walionao ni kuhakikisha wanawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa mazingira.
Sophia amesema hatua ambayo wameichukua kwa hivi sasa ni kuwakutanisha wadau wa mazingira pamoja na maafisa kutoka serikalini kwa lengo la kujadiliana na kupata azimio moja ambalo litafanyiwa kazi mashirika yote 6 yaliyoungana.
Kwa hivi sasa katika kuhakikisha uhamasishaji unayafikia makundi yote tunatumia mikutano ya hadhara ili kufanya uhamasishaji kwa jamii, kushirikiana na vyombo vya habari na sekta za Kiserikali zinasimamia masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi”.alisema Sophia
Kwa upande wake Franklin Kamalamo kutoka Taasisi ya Mazingira Bora amesema Katika kuhakikisha kampeni hii ya kupambana na changamoto za tabia nchi inaleta matokeo chanya watatoa elimu kwa pamoja wadau wote wa mazingira na hii itasaidia elimu kufika kwa urahisi.
Safari hii tunaamini elimu itafika kwa urahisi kwa kuwa jamii tayari inaona mabadiliko mfano kuongezeka kwa joto, maeneo ya joto kupata baridi kali hivyo nirahisi wananchi kuelewa tunachokisema lakini pia tutatumia wasanii kufikisha ujumbe kwa wananchi”.alisema Franklin
Nae Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Mikono Yetu Organization Maimuna Kanyamala amesema katika kampeni hii wataelekeza nguvu kubwa pia kwenye shule za msingi ambao ni watumiaji wakubwa wa miti ili wajue umuhimu wa kupandamiti kunakoendana na matumizi yao ya kila mwaka.
Katika kujenga tabia lazima tuwaguse na hawa wenzetu wa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapanda miti na ikiwezekana lazima kila mwanafunzi awe na mti wake hii itasaidia utunzaji wa mazingira”.alisema Maimuna.
Mtandao wa kijinsia na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania umejidhatiti kuhakikisha unatoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi na kwa sasa mtandao unaendelea na kampeni ya kuielimisha jamii kwa njia mikutano ya hadhara,kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
0 Comments