Na Fadhili Abdallah,Kigoma
AJALI ya barabarani iliyotokea kwenye kijiji cha Kilemba wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imeua watu wanane waliokuwa wakisafiri na gari ndogo aina ya Probox Succeed maarufu kama mchomoko ambapo watu wengine sita wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma leo alisema kuwa Ajali hiyo imetokea tarehe 23 Desemba majira ya saa 11 jioni ambapo watatu wanane wamefariki dunia papo hapo baada ya gari waliyokuwa wakisafiri kugongana uso kwa uso na gari ya kampuni ya CHICCO inayotengeneza barabara ya kiwango cha lami kutoka Kibondo Mjini hadi Mabamba mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Andengenye alisema kuwa hadi kufikia asubuhi leo miili ya watu sita ilikuwa imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao na kwamba hadi sasa miili ya watu wawili bado ipo hospitali ya wilaya Kibondo na watu wameombwa kufika hospitalini hapo kuitambua miili hiyo.
Waliofariki kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni Pamoja na dereva wa gari ndogo Hamisi Chaurembo (27),Bernadina Reuben (22), Madua Asukile, Ntiganiza Bihezako (67), Vedastus Paul (28), Vladmir Vedastus (1) marehemu wengine wawili ambao majina yao hayajatambuliwa hadi sasa.
Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni Pamoja na dereva wa gari la CHICCO, Flavian Felishian (28) aliyejeruhiwa kichwani na kifuani, Juma Saidi (27), Daniel Samwel (33), Silvanus Muhigwa (43) Sara Bundala na Dori Mafumbo (22) ambapo watu watatu watapelekwa hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.
Mkuu huyo wa mkoa ametumia nafasi hiyo ya Mkutano wake na waandishi wa Habari kutoa pole kwa ndugu wa marehemu na kuwataka watu wote mkoani humo kuchukua tahadhari barabarani hasa wakati huu wa likizo ya mwisho wa mwaka ambao umekuwa na ongezeko kubwa kwenye vyombo vya usafiri.
Kamanda wa polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu ambaye alitembelea eneo la tukio alitaja gari zilizohusika na ajali hiyo kuwa ni T 833 DUA aina ya FAW mali ya kampuni ya CHICCO na gari ndogo aina ya Toyota SUCEED yenye namba za usajili T 890 DYZ mali ya Hamisi Chaurembo dereva wa gari aliyefariki kwenye ajali hiyo.
Kamanda Makungu alisema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa dereva wa gari ndogo na ambaye alishindwa kulimudu gari hilo kwenye kona kali hivyo kugongana uso kwa uso na gari hilo la CHICCO.
0 Comments