WAANDISHI wa habari za mtandaoni wametakiwa kufanya kazi kwa manufaa ya Umma pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma zao, hususani katika wakati huu ambao Sayansi na Teknolojia inakua kwa kasi ili kuweza kuyafikia malengo yao.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC,) Kenneth Simbaya, pamoja na kuwataka waandishi wa habari kujiunga kupitia mwavuli wa taasisi ya Tanzania Online Media Alliance (TOMA,) ambao ni mtandao wa waandishi wa habari za mtandaoni nchini ili kujijenga kitaaluma, na kuwa na sekta moja ya waandishi wa habari za mtandaoni yenye sauti moja ya kutetea maslahi yao.
Simbaya, amesema, Uzinduzi wa mpango mkakati wa mtandao wa waandishi wa habari za mtandaoni (TOMA) umelenga kuwaunganisha wanahabari hao pamoja na kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazoendana na wakati, kuzingatia ubora pamoja na kuwawezesha kukuwa kiuchumi.
"Sayansi na Teknolojia inakua kwa kasi, lazima tuzingatie nidhamu katika kufikisha ujumbe na kuzingatia weledi na sheria za habari, pia nichukue fursa hii kuzipongeza klabu za waandishi wa habari za mikoa yote kwa jitihada mnazochukua katika kuimarisha zaidi tasnia hii ya habari, lakini zaidi klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha ambako imetoka taasisi hii ya TOMA." Amesema Simbaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Freedom House ambao ni wadhamini wa mradi huo Daniel Lema amesema kuwa, lengo la kuzindua mpango mkakati huo ni kutoa mwelekeo wa namna ya utekelezaji wa shughuli za taasisi ya TOMA kwa miaka mitano ijayo.
Aidha ameeleza kuwa TOMA imelenga kuboresha habari zinazotolewa na waandishi wa habari za mtandaoni kwa kuhakikisha zinahusisha sauti za pembezoni ambazo hazisikiki katika uga huo ikijumuisha makundi mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia na watu waliopo pembezoni ambako sauti zao hazisikiki na kuhakikisha zinaletwa katika uga wa habari za mtandaoni.
Pia ametoa mwito kwa waandishi wa habari za mtandaoni kujiunga na chombo hicho ambacho kimeundwa kwa ajili yao na kuwataka wajiunge kwa manufaa ya kujijenga kitaaluma, kutoa na kujibu changamoto zinazowakabili.
0 Comments