IMEELEZWA kuwa ili mtoto afikie ndoto zake lazima jamii imuwekee ulinzi awe salama kwa kupinga vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na baadhi ya watu.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta alipokuwa akizindua mradi wa Usalama wa Watoto (UWAWA) awamu ya pili unaosimamiwa na Christian Social Services Commission (CSSC).
Mchatta amesema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi ambapo jamii inatakiwa kuwalinda kwani nao wana ndoto zao za kuwa nani katika jamii mara wamalizapo masomo yao.
"Mradi wa uwawa una lengo la kuimarisha usalama wa watoto utasaidia kuanzishwa dawati la kushughulikia changamoto za watoto kukabiliana na ukatili kwa watoto shuleni na sehemu yoyote wawapo watoto," amesema Mchatta.
Naye Ofisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa kuna baadhi wazazi wanawafanyia vitendo hivyo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwanyima chakula na watoto hujikuta wakifanya vibarua ili wapate fedha na baadhi wazazi wanawauza watoto wao kwa wanaume.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki wa (CSSC) Makoye Wangeleja amesema kuwa wanaushukuru mkoa kwa kutoa ushirikiano kwani vita hiyo siyo lelemama ambapo inabidi kujipanga ili kukabili vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto na watafuata taratibu ili kuweka misingi mizuri ya kuwalinda watoto.
0 Comments