Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu kuanzia mwezi Novemba 2023 hadi April 2024 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa TMA Dkt, Ladislaus Chang'a amesema kuwa, kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ukilinganisha na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024), uwepo wa El-Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu.
"Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa.
Amesema kuwa, athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, vile vile, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka,huku akitoa ushauri kwa wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasimali maji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alifafanua kuwa Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) utabiri wake ulitolewa tarehe 24 Agosti, 2023. Mvua hizo zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa.
Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023. Vilevile, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024.
Aidha TMA imetoa tahadhari kwa makundi na sekta mbalimbali kwenye jamii ikiwemo sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Uvuvi,Utalii na Wanyamapori,Usafiri na Usafirishaji, Nishati, Maji na Madini, Mamlaka za Miji na Wilaya,Sekta ya Afya ,Sekta Binafsi na Menejimenti za Maafa kuchukua tahadhari na kufuatilia utabiri na tahadhali zote zinazotangazwa na TMA kupitia vyombo vya habari ama kwenye kurasa rasmi za mitandao ya Mamlaka hiyo ili kuepukana na Athari za mafuriko na maafa ya mvua.
0 Comments