KUFUATIA hukumu iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa kwa kumfunga jela miaka 22 Mariam Ngoda kwa kosa la kukutwa na vipande 12 vya nyama ya Swala kinyume na Sheria chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kanda ya Iringa kimeanzisha mchakato wa kumsaidia kisheria mjane huyo .
Mwenyekiti wa TLS kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile pamoja na Wakili Cosmas Kishamawe walisema kwa kushirikiana na mawakili wengine wa mkoani Iringa tayari wameanzisha mchakato wa kumsaidia kisheria mjane huyo.
Walisema tayari mchakato wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Mkoa wa Iringa umeanza rasmi Toka Leo asubuhi ikiwa ni muendelezo wa mpango wao wa kutoa msaada wa ushauri na utetezi wa kisheria kwa makundi mbalimbali ya kijamii yasio na uwezo.
Wakili Ambindwile alisema toka waanzishe mpango wa kutoa msaada wa ushauri wa kisheria mkoani Iringa wameendelea kupokea maombi kutoka kwa makundi ya watu wasio na uwezo kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Iringa.
“Tuishukuru sana kampuni ya Asas kwa ahadi yake iliyotolewa na mmoja wa wakurugenzi wake Ahamed Asas kwa kujitokeza kushirikiana nasi ili tuweze kuwafikia watu wengi zaidi wasio na uwezo hususani wale waishio vijijini,” alisema.
Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 3, mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu Mkoa wa Iringa Said Mkasiwa baada ya kujiridhisha kuwa ni kweli mjane huyo mwenye watoto wanne alikutwa na ndoo iliyokuwa na nyama hiyo yenye thamani ya Sh 900,000 kinyume na Sheria .
Akitoa hukumu hiyo kwa mjane huyo mkazi wa Zizi la Ng’ombe mjini Iringa, Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, Mkasiwa alisema kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (c) cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba tano ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 59 (a) (b) cha mabadiliko ya sheria ya mwaka 2016.
Wakati akijitetea bila usaidizi wa wakili mjane huyo alikiri ni kweli alikutwa na ndoo yenye nyama hiyo ambayo alidai alikabidhiwa na mtu aliyemtambua kwa jina moja la Fute bila kujua ina nyama ya nini .
Alisema alilazimishwa abebe ndoo hiyo na kufikishwa kituoni na kufunguliwa kesi ya kukutwa na nyara za serikali sambamba na kosa la uhujumu uchumi.
Hukumu hiyo imekuwa ikijadiliwa kwa Nguvu sana kwenye mitandao ya Kijamii na kuibua mijadala mizito .
0 Comments