Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Naibu wa Rais Mstaafu wa Afrika ya kusini Phumzile Mlambo Ngcuka amesema ili ukatili wa kijinsia umalizike ndani ya jamii ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wanaume pamoja na kutoa elimu wa kutoa taarifa wa vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua.
Kauli hiyo, ameitoa jijini Dar es Salaam katika Tamasha la 15 la jinsia, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka 30 ya tokea kuanzishwa kwa Mtandao wa Jinsia nchini TGNP ambapo ameipongeza TGNP kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambo dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu kwenye jamii na kishirikisha makundi yote.
"Nitoe changamoto kwa TGNP katika mikutano kama hii kuwepo na kundi la wanaume na washirikishwe hatua kwa hatua katika harakati za kupinga ukatili lwa kijinsia ili kufikia malengo ya kuwa na jamii yenye usawa kwa wakati".
Ameongeza kuwa, kabla ya mkutano wa Beijing China madhila mengi waliyokuwa wakifanyiwa wanaweke yalikuwa hayana mipaka na vigumu kushughulika nayo lakini baada ya mkutano mataifa yaliweza kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wake ambayo mengi yao ikiwemo Tanzania hivi sasa yamepiga hatua kubwa katika kupinga ukatili wa kijinsia.
"Tumetoka mbali hatuna budi kujipongeza lakini hatupaswi kumpumzika, kazi bado ipo ya kubadilisha Dunia" amesema Phumzile.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Liliani Lihundi amesema Tamasha la Jinsia limekuwa chachu kubwa ya kuleta sauti ya pamoja na zaidi kutoa fursa kwa wanawake wa mashinani kupaza sauti zao, ni jukwaa la kipekee kwa Tanzania linaloleta wadau wengi kwa pamoja na kuwapa fursa ya kuwa na sauti ya pamoja.
"Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 jukwaa hili limeweza kuwaleta pamoja takribani watu 35,000, asilimia 70 wakiwa ni wanawake" amesema Liliani
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Women Fund amesema huwezi kuzungumzia mafanikio ya wanawake bila kuzungumzia wanaharati na Taasisi zinazoshughulikia usawa na haki za kijinsia.
"Wanaharakati wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutoa Elimu na kujenga uelewa kwa jamii ya kuweza kuachana na ukatili wa kijinsia. Wamewawezesha wanawake kujitambua na kuweza kupambania haki zao".
Aidha ameipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kukubali kuibeba agenda ya ukatili wa kijinsia.
Tamasha hilo limeanza November 7 na linatarajiwa kuhitimishwa November 10/2023 katika viwanja vya TGNP Mabibo.
0 Comments