Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
SHIRIKA Lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL) kwa ufadhiri wa Taasisi ya MO Dewji Foundation limefanikiwa kukarabati na kuvifufua visima 38 ambavyo baadhi vilikuwa havitowi maji vilivyopo katika kata 12 za Manispaa ya Singida kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.
Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo linalojishughulisha na kubadili maisha ya jamii,Joshua Ntandu alisema jana kuwa baada ukarabati na ufufuaji huo kukamilika umewawezesha zaidi ya wananchi 38,400 kuondokana na tatizo la uhaba wa maji katika maeneo yao.
Ntandu alisema kabla ya ufufuaji na ukarabati huo kufanyika,shirika hilo lilifanya upembuzi yakinifu na kugundua kuna visima 45 vya maji vilivyochimbwa wakati Mohammed Dewji akiwa Mbunge wa jimbo la Singida Mjini miaka kadhaa iliyopita lakini vilikuwa havifanyi kazi tena kutokana na hitilafu mbalimbali.
“Katika shughuli zetu za kila siku, ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ukeketaji, tuliona suala la afya na usafi kwa wananchi ni suala muhimu na katika kufuatilia suala hilo tulibaini kati ya visima 45 ni visima 38 pekee vinavyoweza kufufuliwa na kukarabatiwa vianze kutoa huduma ya maji kwa wananchi," alisema.
Alisema mpango wa ufufuaji wa visima hivyo ulikuwa ni wa muda mfupi na kwamba mkakati uliopo shirika hilo wamekubaliana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) kuunganisha maji yanayotolewa na mamlaka hiyo kwenye kata ambazo zipo pembezoni mwa mji.
Ntandu alisema mpango huo utasaidia kuongeza mtandao wa upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Singida kutoka asilimia 86.4 hadi kufikia asilimia 96.4 ifikapo mwaka 2026 na kwamba maji ya visima vyote vilivyifufuliwa na kukarabatiwa yalipimwa katika maabara na kubainika yanafaa kwa asilimia 93 kwa matumizi ya wananchi.
Afisa Mtendaji huyo aliongeza kuwa mpango mwingine uliopo ni kwa ESTL na Mo Dewij Foundation kufanya ushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Singida ili kupanua wigo wa upatikana wa maji katika wilaya,kata na vijiji vyote vilivyopo katika mkoa huo kwa kuzingatia sera ya maji ya 2002 ambayo inataka wananchi wapate maji ndani ya mita 400.
Aidha, Ntandu alihimiza umuhimu wa kuvitunza visima hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kutengeneza mpango mzuri utakaotumika kuvifanyia matengenezo vitakapokuwa na changamoto ya kuharibika kwa kuwa wao hawatahusika tena na matengenezo hayo.
Naye Mhandisi wa Maji wa Shirika hilo, Edward Barnaba alisema visima vimekuwa vikiharibika kutokana na kuingia kwa mchanga na watoto kuweka mawe kwenye pampu ya kusukuma maji na kuharibu mfumo wake na kushauri maeneo vilipochimbwa iachwe nafasi ya mita 60 na kuzungushiwa uzio ili mazingira yake yasiharibiwe tena.
Fundi Sanifu Mkuu Ubora wa Maji, Maabara ya Singida, Shifaya Munisi alisema baada ya kupima ubora wa maji baada ya kufufuliwa kwa visima hivyo yameonekana kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Mwakilishi wa Mo Dewji katika ufufuaji wa visima hivyo , Janeth Mashauri, aliwataka wananchi ambao visima vyao vimefufuliwa wavitunze kwani ni mali yao.
Mkazi wa Kitongoji cha Sanga Kata ya Unyambwa, Mwajuma Mohamed alizishukuru taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo na kueleza kuwa licha ya kufufuliwa bado kunachangamoto ya upatikanaji wa maji hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa kitongoji hicho ambapo aliomba kama utakuwepo uwekano wachimbiwe visima vingine.
0 Comments