Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaonya wananchi wanaofanya ujenzi holela katika maeneo ya hifadhi ya barabara pamoja na maeneo hatarisha kuacha mara moja ili kuepuka madhara mbalimbali yanayoweza kuwapata.
Babu ametoa kauli hiyo leo katika kikao cha Bodi ya barabara mkoa (Road board) ambapo alisema kuwa wapo wananchi ambao wamekuwa wakivunja sheria kwa kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kujenga makazi na maeneo ya biashara huku wakitambua wazi kuwa ni kinyume na sheria.
"Watu wanaojenga pendezoni mwa barabara wanaweza kuchangia kutokea madhara makubwa hasa ajali zinapotokea hususani maafa makubwa ya watu lakini pia hupelekea mwingiliano mwa watembea kwa miguu na vyombo vya moto hivyo Tanroad na Tarura mnawajibu wa kuhakikisha hamkubali mtu kuvunja sheria" alisema Babu.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, wapo baadhi ya watu wenye nia hovu wamekuwa wakihujumu kwa makusudi kwa kuiba alama za barabara na kwenda kuziuza kama vyuma chakavu na kuwataka wale wanaofanya hivyo kuacha mara moja.
Alisema kuwa, ipo haja kwa Tanroad pamoja na Tarura kuanza kubuni njia ya kufunga kamera barabarani ili kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaofanya wizi wa alama za barabarani ili waweze kufikishwa mahakamani.
Babu alisema kuwa, kwa sasa kunauharibifu mkubwa wa barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwapongeza Tarura na Tanroad kwa jinsi wanavyojitahidi kuhakikisha barabara zote zinapitika kipindi hiki.
"Niendelee kuwaagiza Tanroad hakikisheni dosari zinazotokea katika barabara kuu kipindi hiki cha mvua zinakarabatiwa haraka ili kuepukana na ajali na nimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasani kwa jinsi ambavyo anatoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara za mkoa" alisema Babu.
Kwa upande wake, Meneja wa Tarura mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Nicholous Fransis alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23 Tarura Kilimanjaro iliidhinishiwa Bilioni 33.645 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara.
Mhandisi Fransis alisema kuwa, katika mwaka huo wa fedha Tarura ilitekeleza miradi 80 yenye thamani ya Bilioni 32.974 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98.
Alisema kuwa, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 Tarura Kilimanjaro imeidhinishiwa Bilioni 36.041 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara na madara na jumla ya miradi 85 itatekelezwa.
"Zipo barabara ambazo tumeziombea fedha nje ya bajeti ambazo barabara hizo ni muhimu na nyingine ni za ahadi za viongozi ambapo kwenye mwaka wa fedha 2023/24 tumeomba Bilioni 92.687" Alisema Mhandisi Fransis.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanroad mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando alisema kuwa, kwa upande wa Tanroad katika mwaka wa fedha 2023/24 wametengewa zaidi ya Bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara.
Mwisho.











0 Comments