Header Ads Widget

POLISI IRINGA WANAMSAKA BABA ALIYEUA MTOTO WAKE KWA KUMNYONGA HUKU AKIJIPIGA PICHA

 

JESHI   la  Polisi  mkoa  wa  Iringa   linaendelea   kumtafuta  kijana  Goodluck Mgovano mkazi  wa mtaa wa  Mlandege  Kota  katika Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa anayetuhumiwa   kumuua kwa  kumnyonga  kwa kamba shingoni  mtoto  wake  Alvin Mgovano mwenye  umri  wa  miaka  miwili  na nusu  kutokana na kurushiana  maneno kati yake na mama  wa  mtoto .

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mama mlezi wa mtoto huyo  Magdalena Luvanda alisema   kuwa baba mzazi wa mtoto Alvin alifika eneo ambalo mama mzazi wa  mtoto anafanyia biashara na kumchukua mtoto huyo kwa lengo la kwenda naye nyumbani na  ndipo alipofanikiwa kutenda tukio hilo la kikatili.

Baada ya kutenda tukio hilo la kumnyonga mtoto wake kwa kutumia kamba aliyoifunga katika mlango wa nyumba, baba mzazi wa mtoto huyo anayefanya kazi ya utingo wa magari ya mizigo, alijipiga picha mbili katika simu yake akiwa anamnyonga mtoto na  picha  nyingine  alimpiga mtoto baada ya kumnyonga na picha nyingine alijipiga yeye pamoja na mtoto huyo (selfie) na kuandika ujumbe mfupi kwamba amemuua kwa sababu yeye ndiyo amemleta duniani na yeye ndiye anayemtoa pia ameagiza mtoto huyo azikwe pale atakapozikwa yeye.


Diwani wa kata ya Mlandege Wakili Jackson Chaula  akizungumzia  tukio hilo alisema  kuwa tukio  hilo  ni la kwanza  kutokea kwenye kata  yake na  kuwataka  wananchi  kuepuka na  visasi  kama  hivyo na hata kama kuna  ugomvi  wa  kifamilia  ni  vema  kuumaliza  kwa amani  kuliko  kufanya ukatili kama huo.

Kamanda  wa polisi wa  mkoa wa  Iringa  Allan Bukumbi aliwaeleza  waandishi  wa habari Leo   ofisini  kwake  wakati  akitoa  taarifa  za matukkio  mbali mbali ya uhalifu ndani ya  mkoa   wa  Iringa   kuwa  tukio   la  kijana  huyo  kumnyonga  mtoto  wake  lilitokea majira ya  jioni  Ijumaa Octoba  20 mwaka  huu.


"Inasemekana   kijana   huyo alichukizwa na maneno  waliyorushiana na mzazi  mwenzake  hivyo kupelekea  hasira   zake  kwa  kuua  mtoto wake  na kuacha  ujumbe  wa maandishi  kuwa  mtoto  huyo azikwe  atakapozikwa  yeye,hadi    sasa  bado  tunaendelea  kumtafuta   kijana   huyo " alisema kamanda  Bukumbi .

Katika  hatua  nyingine  kamanda  Bukumbi  alieleza  mafanikio  mbali mbali ambayo   jeshi  hilo  imeyapata  kutokana na  kuwakamata  watuhumiwa mbali mbali  wakiwemo  wa  ubakaji ambapo  baadhi ya kesi  zimehukumiwa mahakamani  ikiwemo  kesi ya  Suleman  Wabuha (78) mkulima  wa kijiji cha Idodi  wilaya ya  Iringa aliyehukumiwa  kifungo  cha maisha  jela na  kumlipa fidia  muhanga  kiasi cha  shilingi milioni 5 kwa  kosa l;a kubaka  na kumuambukiza virusi vya UKIMWI  muhanga .

Watuhumiwa  wengine  ni pamoija na Doto Kisinga (36) mkulima  wa  Ulata  wilaya ya  Iringa aliyehukumiwa kifungo  cha maisha  jela na kumlipa  fidia muhanga ya shilingi  milioni 5 kwa  kosa la  kubaka  pia  Richard Kinyamagoha (20) mkulima  na mkazi  wa  Lukani wilaya ya  Kilolo aliyehukumiwa  kifungo  cha miaka  30 jela  pamoja na kutakiwa  kulipa   fidia ya  shilingi 300,000 kwa  kosa la  kubaka.


Aidha  Kamanda  Bukumbi  alitaja  watuhumiwa  wengine  waliopatikana na hatia na kufungwa kuwa ni Erick Kisoma (28) mkazi  wa  Mkalanga  wilaya ya  Kilolo  aliyehukumiwa kifungo  cha miaka 30  jela pamoja na kutakiwa  kulipa fidia ya  shilingi 500,000 kwa  kosa la kubaka  pamoja na Dickson Mkana  (30) mkulima na mkazi wa kijiji cha  Igowole  wilaya ya  Mufindi aliyefungwa  jela  miaka  mitatu na kutakiwa  kulipa  faini ya  shilingi 300,000 kwa  kosa la  wizi  wa  pikipiki.

Katika  hatua  nyingine kamanda  Bukumbi  alisema jeshi  la polisi  mkoa  wa Iringa  katika  oparesheni  iliyofanyika  kuanzia  Oktoba  mosi  hadi Oktoba 30  lilifanikiwa  kumkamata  mtuhumiwa  mmoja  aliyefahamika kwa  jina la Adam Mgunda (29) mkazi  wa Ilula kwa  kosa la  kupatikana na nyara  za  serikali  ambazo ni  meno ya  Tembo  vipande vitano  ambavyo  alikuwa amehifadhi  kwenye mfuko  wa  sandarusi  akiwa anasafirisha  kwa  kutumia usafiri wa pikipiki .

Tukio  jingine ni la   Oktoba 28  katika  kijiji cha Kidamali  wilaya ya  Iringa  kando kando ya  barabara  kuu ya kwenda  Hifadhi ya  Taifa ya  Ruaha  ambapo  jeshi la  polisi kwa kushirikiana na askari  wa wanyamapori  walifanikiwa  kukamata  vipande 25 vya meno ya  Tembo ambavyo  vilitelekezwa na mtu /watu  wasiojulikana vipande  hivyo  vilikutwa kwenye  mifuko  mitatu ya Sulphate uchunguzi  unaendelea  ili  kuwabaini  wahusika .

Wakati  huo  huo  jeshi la  polisi  limekamata silaha  aina ya Gobore  iliyotengenezwa  kienyeji  iliyotelekezwa  katika shamba la David Mgava kijiji  cha Kisovela  kata ya Nduli  Manispaa yab  Iringa .

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI