Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amezitaka kampuni zinazosimamia miradi ya umeme nchini Tanesco na Wakala wa Nishati vijijini (REA) kununua vifaa vya umeme vinavyozalishwa hapa nchini ili kukuza viwanda vya ndani, kuvipa thamani na kukuza ajira pamoja na uchumi wa Nchi.
Ametoa agizo hilo leo Novemba 15,2023 wakati wa ufunguzi wa umeme wa ujazilizi katika maeneo ya vijiji – miji awamu ya III mitaa ya Pachoto A, Pachoto B na Pwani kata ya Naliendele mkoani Mtwara.
“Wito wangu kwa Tanesco na REA mchezo wa kununua vifaa nje ya nchi wakati ndani tuna viwanda hapa ndani nayo zilipendwa, eti jamani tuna kiwanda cha wire kiko hapo unaacha unaenda kununua Nchi fulani unataka nini, hivi viwanda atanunua nani kuanzia leo vifaa vinavyopatikana ndani ya nchi vinunuliwe hapa na zinazopatikana nje ya Nchi vitanunuliwa huko. Amesema Dkt.Biteko
Sambamba na hilo amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia vyema kazi ya kusambaza umeme, amewataka kutokucheka na wakandarasi hao ili kazi ya kupeleka mahitaji ya umeme kwa wananchi ifanyike kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Jones Olotu alimweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa, Mkoa wa Mtwara umetengewa shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini na kwamba katika vijiji 785 vya mkoa huo, Vijiji 401 bado havina umeme lakini wakandarasi kampuni ya Derm, Central na Namis wanaendelea kusambaza umeme kwenye Vijiji vilivyosalia.
0 Comments