Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Watu wawili wakazi wa kitongoji cha Mushenyi kata ya kalinzi wilaya ya kigoma wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa, kuporwa na kuharibiwa kwa mali zao kulikofanywa na baadhi wananchi wa kijiji hicho wakiwawatuhumu kujihusisha na vitendo vya imani za kishirikina.
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Gaston Kabage akieleza tukio hilo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya kigoma amesema kuwa vitendo alivyofanyiwa si vya kiungwana na wanakijiji wenzao kwa madai ya kuwabaini kuwa wao ni wachawi kupitia upigaji wa ramli.
Alisema kuwa alinusurika kuuawa baada ya kutoroka kupitia mlango wa nyuma kufuatiwa wanakijiji wenzake kuvunja mlango wa mbele wakitangaza kumsaka huku wakiwa na mapanga na Marungu.
Kwa upande wake mtoto wa mwenye nyumba hiyo,Dainesi Gaston alisema aliona kundi kubwa la watu linavamia nyumba yao kwa kurusha mawe juu ya bati, kuvunja vioo vya madirisha na kukatakata migomba hivyo alipiga kelele kumwita baba yake ili ashuhudie hali hiyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Salumu Kali ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo amekemea vitendo hivyo na kutangaza kuwa serikali itachukua hatua madhubuti kwa wale wote waliohusika na kushiriki kwenye vitendo hivyo.
Kali alisema kuwa kupitia kamati ya ulinzi ya wilaya wameanza kubaini waliotajwa kuhusika na vurugu hizo na kwamba watatembea nyumba lwa nyumba kuwakamata wahusika.
0 Comments