![]() |
Prof. Aldof Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia |
Na Hamida Ramadan Matukio daima AAP Dodoma
Wamiliki wa Shule binafsi nchini wameiomba Serikali kuliwekea mkazo suala zima la Mmonyoko wa maadili na hivyo kutaka somo la dini kuanza kufundishwa elimu ya awali kama msingi muhimu wa kujenga maadili ya wanafunzi.
Ombi hilo limekuja baada ya serikali kuitisha kikao baina ya serikali na wamiliki wa shule binafsi ili kujadili changamoto zinazowakabili.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dodoma Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema katika kikao hicho wamepokea maoni kutoka kwa wamiliki hao wa shule binafsi na lengo ni kuona ni jinsi gani wanarudisha maadili Kwa watoto .
Wamiliki hao wamesema ufundishwaji wa Somo la dini kuanzia elimu ya awali ndio msingi muhimu wa kujenga maadili Kwa watoto wetu wa sasa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga alisema kuwa wameyachukua mawasilisho yote yaliyowasilishwa na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kwani isingekuwa kazi rahisi kujibu kila kilichoelezwa katika mkutano huo.
Alisema kuwa Serikali ni sikivu na imeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto na kusema kuwa huo ni mwanzo hivyo wamepata sehemu ya kuanzia.
"Huu ni mwanzo tu na sio kikao chetu cha mwisho na ilikuwa ni lazima tupate pa kuanzia ameshazungumza kamishna hapa kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na kwavile jambo hili ni mtambuka linahitaji Uratibu na ushirikiano wa Wizara zingine,
Tunawahitaji watu wa Wizara ya fedha tuwe nao hapa, tunawahitaji pengine watu wa Katiba na sheria tufanye nao kazi tunahitaji watu wa Wizara ya utumishi sababu kuna masuala ya kiutumishi hapa yamezungumzwa hao wote wanahitajika ili tuweze kupata muelekeo ambao ni sahihi,"alisema
Aidha amesema kuwa kupitia mkutano huo wanaanza kutengeneza muelekeo mpya na katika kikao kijacho wataanza na kuzitatua changamoto walizozijadili katika mkutano huo na kuweza kujua ni wapi wamefikia.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Aldof Mkenda amesema kuwa Sekta binafsi kwenye Serikali sio mshindani bali ni mshiriki wa Serikali hivyo Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi.
Waziri huyo amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi na inathamini hivyo watahakikisha wakiwapa ushirikiano katika kutatua changamoto zinazowakabili.
"Huu ni mwanzo tutakapo kutana Machi mwaka kesho tutakuwa tayari tumepata pakuanzia na kuona ni changamoto zipo bado hazijatatuliwa,"amesema.
0 Comments