Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima APP.
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza programu na mipango mbalimbali ya Elimu ya Watu Wazima nje ya mfumo rasmi.
Hatua hiyo ina lengo la kuwa na Watanzania walioelimika na wenye uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,.Josephat Luoga wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya wiki
ya Elimu ya Watu Wazima wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Luoga amesema miongoni mwa program hizo ni pamoja na Mpango wa Elimu Msingi kwa walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Elimu Sekondari kwa njia Mbadala (AEP).
Nyingine ni Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya shule (IPOSA).
"Program nyingine ni Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu na Jamii (MUKEJA), Uzalishaji Mali (UMALI), Shughuli za Ugani (SU) pamoja na Village Community Bank (VIKOBA).
"Serikali inawatarajia washiriki na wadau kuchangia kwa tija mijadala mbalimbali katika kongamano hilo ili iweze kuisaidia kuja na afua stahiki zitakazo imarisha utolewaji wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi." amesema Luoga na kuongeza kuwa:
"Kupitia mijadala hii ya leo tunaweza kupata fursa nzuri ya kuinua kiwango cha kujua Kusoma, Kuandika na na Kuhesabu kwa vijana na watu wazima, wanawake na wanaume ili nguvu kazi hii iweze kuchangia katika kuinua pato la nchi na mtu mmoja mmoja" amesema Luoga.
Kuhusu historia ya Maadhimisho hayo, Luoga amebainisha kuwa tangu mwaka 1961, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi mahususi katika kukabiliana na tatizo la kutojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
"Katika mwaka 1970 Mwalimu Julius Nyerere alitumia Elimu ya Watu Wazima kuzindua kampeni mbalimbali, ikiwemo Kisomo chenye nanufaa (KCM), pamoja na program saidizi za kisomo kama vile Elimu Kwa Wafanyakazi" amefafanua Luoga.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kongamano hilo Dk. Sempeo Siafu amesema maadhimisho hayo yaliasisiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 1966 ili kuikumbusha jamii umuhimu wa Elimu ya watu wazima, na kulitambua kama suala la heshima na haki za binadamu.
"Hapa Tanzania tumekuwa tukiadhimisha katika ngazi ya mkoa au wilaya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazotekeleza program za Elimu ya Watu Wazima" alibainisha Dk. Siafu.
Dkt. Siafu ameongeza kuwa Wizara ya Elimu imeandaa Miongozo mitano ambayo itasaidia katika utekelezaji wa kuimarisha Ubora wa utolewaji wa Elimu ya Sekondari kwa Njia mbadala (AEP), mpango unaolenga kuwapa fursa ya kuendelea na masomo vijana walio nje ya mfumo rasmi hasa wasichana waliopata ujauzito.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima 2023 yamelenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wote pamoja na kupaza sauti kuhusu umuhimu wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kwa jamii.
Awali Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Profesa Michael Ng'umbi amesema Taasisi inatambua kuwa tangu 1960 mpaka sasa Tanzania imekuwa tofauti kwani pamoja na kuendelea na juhudi za kusoma na kuandika, sasa jamii inatilia mkazo kupambana na Mabadiliko.
0 Comments