Na Thobias Mwanakatwe,Singida
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) kupitia mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa pili imejiwekea lengo ifikapo Juni 2024 vijiji 4,072 vitakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme na hivyo kufanya jumla vijiji vyote 12,318 vilivyopo Tanzania Bara vitakuwa vimepata nishati hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili unaovihusisha vijiji 120 vya Wilaya ya Iramba mkoani Singida ambao ulifanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema utekelezaji wa mradi huo kwa vijiji vilivyobaki utagharimu Sh.Trilioni 1.6 na kwamba mpaka sasa vijiji 11,000 vina umeme na vijiji 1300 vilivyobaki vitafikiwa na umeme ifikapo Juni 2024.
Saidy alisema REA tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umesaidia kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kwa upande wa Tanzania Bara kutoka asilimia 5 mwaka 2007 hadi 70 mwaka 2020 tathimini ya mwisho ilipofanyika.
Aidha, alisema kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo nchini, vitongoji 28,659 sawa na asilimia 44 vishafikiwa na huduma ya umeme.
Alisema Serikali inaendelea na mipango ya kuongeza mafungu katika Mfuko wa Nishati Vijijini ili kuongeza kasi ya kufikisha umeme katika vitongoji 36,101 vilivyobaki kupitia Mpango wa Kufikisha Umeme Vitongoji Vyote (Hemlet Electrification Project-HEP).
Aliongeza kuwa mbali na shughuli za uchumi na huduma za jamii, umeme vijijini umesaidia kuboresha ulinzi, kuhifadhi mazingira, kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuchangia azma ya serikali katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambapo upatikanaji wa nishati bora utasaidia kufikia malengo 13 kati ya malengo 17.
" Hivi tunavyoongea serikali yako inatekeleza miradi mikubwa saba ya kupeleka umeme maeneo ya vijijini kupitia kandarasi 112 (Contract/Lots) ambayo kwa ujumla wake itapeleka umeme katika vijiji na vitongoji takribani 11,000," alisema.
Saidy alisema mradi huu wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili ndio unaenda kuhitimisha safari ya kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote 12,318 Tanzania Bara kama ambavyo imeelekezwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 kuwa ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote viwe vimefikiwa na huduma za umeme.
Naye Rais Samia akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo, alisema Wilaya ya Iramba ni sehemu ya mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao unalenga kufikia vijiji 178 vilivyopo katika wilaya za Singida vijijini,Mkalama,Manyoni,Ikungi na Iramba.
"Asilimia 90 ya kazi yote imekamilika na tunatarajia katikati mwakani (2024) mkoa wa Singida wote utakuwa unawaka umeme," alisema.
Rais Samia alisema serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu za kuimarisha gridi ya taifa ili kuondokana na kero ya umeme kukatikatika mara kwa mara.
0 Comments