Header Ads Widget

HII HAPA MIKATABA UJENZI WA MELI ZIWA TANGANYIKA





Eric Hamis: Mkurugenzi Mtendaji - MSCL



Na Fadhili Abdallah, Kigoma

 

 

Shirika la huduma za Meli nchini (MSCL) na Kampuni ya DearSan  ShipYard ya Uturuki zimetiliana saini mikataba mitatu yenye thamani ya shilingi bilioni 630 ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza meli na ujenzi wa meli mbili za mizigo katika ziwa Tanganyika na ziwa Victoria ukiwa ni utekelezaji wa mpango wa serikali kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa ajili ya soko la nchi za maziwa makuu.

 

Waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa ameshuhudia Utiaji saini wa miradi hiyo  kwenye bandari ya Kigoma mjini ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL, Eric Hamisi alisema kuwa mradi wa kwanza utahusisha  ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza meli (chelezo) utakaojengwa kwenye eneo la Katabe Manispaa ya Kigoma Ujiji utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni  322.7  ukitarajia kuchukua miezi 24 kukamilika.

 

Sambamba na mradi huo Hamisi alisema mkandarasi huyo pia atatekeleza mradi wa ujenzi wa meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba mabehewa 25 ya treni kila behewa likiwa na uzito wa tani 140 hivyo kufanya meli hiyo itakayofanya kazi kwenye ziwa Tanganyika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 3500 ikitarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni  158.2 ambapo mradi huo unatarajia kuchukua miezi 36.

 

Aidha Mkurugenzi huyo wa MSCL alisema kuwa utiaji huo saini unahusisha pia ujenzi wa meli ya mizigo kwenye ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeta tani 3000 ikitarajia kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 145 ukitarajia kutumia miezi 24 kukamilika na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutakuwa ukombozi mkubwa wa shughuli za biashara na uchumi kwa mikoa inayopakana na ziwa Tanganyika na nchi kwa ujumla.


Prof. Makame Mbarawa – Waziri wa uchukuzi Tanzania


Akizungumza kabla kutiwa saini kwa mikataba hiyo Waziri wa uchukuzi,Prof.Makame Mbarawa alisema kuwa miradi hiyo ni utekelezaji wa mipango ambayo serikali ya awamu ya sita imeiweka ya kutumia mkoa wa Kigoma kwenda  eneo la nchi za Maziwa makuu kama kitovu cha biashara.

 

Mbarawa alisema kuwa miradi hiyo italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi ambapo ameitaka MSCL kusimama imara katika usimamizi wa miradi hiyo lakini kubuni mikakati ambayo itafanya kiwanda cha meli kupata wateja kutoka nchi za DRC na Burundi sambamba na meli zitakazotengenezwa kupata mzigo wa kutosha utakaoliingizia taifa fedha.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI