Na,Jusline Marco;Arusha
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt.Husein Ali Mwinyi amezitaka nchi na Serikali zote wanachama wa Umoja wa Afrika kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto zinazo kabili suala la ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu katika bara la Afrika.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 20 katika ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kilichofanyika jijini Arusha na kuzitaka Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu, AZAKI na wadau wengine kufahamu haki za binadamu wanazozitetea.
Aidha amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutekeleza na kusimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha haki za binadamu na watu zinalindwa,Serikali ilianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa lengo la kutetea,kulinda na kuhifadhi haki za binadamu nchini ambapo katika katiba ya nchi haki za binadamu ibara ya 12 hadi 24 imeainisha wajibu wa kila raia.
Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa Serikali mbalimbali na Taasisi za haki za binadamu kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na kushughulikia kikamilifu changamoto zilizopo na nchi za Afrika kuendelea kushirikiana katika kuyakabili matukio mbalimbali yanayohitaji msaada wa kibinadamu katika Bara letu.
Ameeleza kuwa Serikali imechukuwa jitihada mbalimbali ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa Mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama ambapo kwa kiasi kikubwa, jitihada hizi zimeboresha hali ya upatikanaji wa haki ikiwemo haki ya usawa mbele ya sheria, afya, elimu, maji na mazingira safi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, ajira, haki ya kumiliki mali na uhuru wa vyombo vya habari.
"Kutokana na uhuru huo, hivi sasa Tanzania ina vyombo vya habari vingi vikiwemo redio 210, televisheni 56, magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii na tumefikia hatua kubwa ya kuimarika kwa uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia."Alisisitiza Dkt.Mwinyi
"Sote tunafahamu kuwa suala la ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu katika bara la Afrika kwa jumla, bado kwa kiasi fulani linakabiliwa na changamoto na Miongoni mwao hizo ni mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.Alisema Dkt.Mwinyi
Vilevile ameainisha changamoto na majanga mbalimbali ambayo bara la Afrika linapitia na wahanga wake wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto ambapo kwa kutambua hilo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua katika kutatua migogoro mbalimbali na kutekeleza kwa vitendo Tamko la Dar es Salaam kuhusu Amani, Usalama, Demokrasia na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
"Katika kuepusha uvunjifu wa haki za binadamu unaotokana na vita, kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania inashiriki katika Jeshi la pamoja la kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kushiriki katika ulinzi wa amani katika nchi mbali mbali ikiwemo Darfur Sudan na Visiwa vya Comoro."Alieleza Dkt.Mwinyi
Sambamba na hayo amempongeza Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Watu kwa uongozi wake imara katika kuiongoza taasisi hiyo muhimu ya Umoja wa Afrika, Taasisi ambayo inalinda, inakuza na kuendeleza haki za binadamu na watu katika Bara la Afrika.
Mkutano huu utajadiliwa masuala mbalimbali ikiwemo hali ya haki za binadamu katika bara la Afrika, taarifa za kazi za Makamishna pamoja na taarifa za mifumo ya ulinzi wa haki za binadamu Afrika ambapo taarifa hizo zitatoa tathimini ya hali halisi ya haki za binadamu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupata mbinu za kukabiliana na changamoto zitakazoainishwa na washiriki watapata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusiana na masuala yatakayojitokeza katika taarifa zitakazo wasilishwa.
"Ni matumaini yangu kuwa taarifa hizi zitatoa tathimini ya hali halisi ya haki za binadamu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupata mbinu za kukabiliana na changamoto zitakazoainiahwa na washiriki watapata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusiana na masuala yatakayojitokeza katika taarifa zitakazo wasilishwa."Alisema Dkt.Mwinyi
Kikao hicho ambacho kilitanguliwa na majukwaa ya Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu zipatazo 46 na Asasi za Kiraia takribani 210 kutoka Bara la Afrika, Taasisi hizi ni wadau muhimu katika masuala ya ulinzi, utetezi na uhifadhi wa haki za binadamu barani Afrika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ya Tume ya Haki za Binadamu na Watu Profesa Lemy Ngoy Lumbu amesema mapendekezo yanayotolewa kila mwaka na Tume hiyo kuhusu haki za binadamu na watu yanafanyiwa kazi kwa asilimia moja ama sifuri na nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika.
Prf.Lumbu amesema mapendekezo ya kutungwa kwa sheria yanapaswa kupelekwa ili kuzitaka nchi hizo kutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo na hatua zitakazochukuliwa kwa nchi zitakazokaidi kutekeleza.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Pindi Chana amesema kama serikali wanaheshimu haki za binadamu ikiwemo makundi maalum ambapo amesema milango ipo wazi ya serikali kupokea maoni na changamoto na kufanya mazungumzo kwa maslahi ya nchi
Msajili wa Mahakama ya Afrika Dkt. Robert Eno akizungumza kwa niaba ya rais wa mahakama hiyo amezitaka nchi za Afrika kutekeleza hukumu zinazoyolewa na mahakama hiyo dhidi ya mashtaka mbalimbali yanayohusu haki za binadamu na kusema kuwa hukumu nyingi zinazotolewa na Mahakama hiyo hazitekelezwi na nchi Wanachama.
Amesema hali hiyo inakwamisha upatikanaji wa haki kwa Wananchi wa Bara la Afrika lakini pia zinachochea uvunjifu zaidi wa haki za binadamu na raia katika nchi mbalimbali ambapo Dkt. Eno amezitaka nchi zilizoridhia uanzishwaji wa mahakama hiyo kutekeleza hukumu zinazotolewa na Mahakama hiyo ili kutoa haki kwa raia wa nchi zao
0 Comments