Na Mwandishi wetu, Mtwara
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt. Stephen Isaac Mwakajumilo amekuja na mkakati mpya wa ujenzi wa mji mpya Mangaka utakaoboresha muonekano wa uso wa mji.
Akizungumza na wafanyabiashara wa Mangaka na Kilimanihewa alisema kuwa Wilaya inaratibu mpango wa ujenzi utakaoboresha muonekano wa uso wa mji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ujenzi wa maghorofa, uwekaji wa taa za barabarani pamoja na kutenga maeneo ya uwekezaji katika ujenzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, Viwanda na Mahoteli.
Mwakajumilo alisema kuwa mpango wa uhamasishaji wa ujenzi wa mji mpya utakakuwa na matokeo chanya huku Serikali ikijikita katika kutekeleza ujenzi wa miundombinu mhimu ikiwemo ujenzi wa soko la Wilaya ya Nanyumbu.
Katika mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa katika miji ya Mangaka na Kilimanihewa, ikiwemo Ujenzi wa Shule Mpya ya Awali na Msingi Kilimanihewa unaogharimu Shilingi Milioni 608.2 na Ujenzi wa Shule ya Kitaifa ya Wasichana Naishero unaogharimu shilingi Bilioni 3.
Miradi mingine ni Ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha Lami ikiwemo barabara ya Likungwa na Msangi yenye urefu wa Kilomita 1.2 unaogharimu Shilingi Milioni 948.5, Mradi wa Maji toka Mto Ruvuma unaogharimu Shilingi Bilioni 38.1 na Mradi wa Maji Sengenya unaogharimu Bilioni 3.6 Hotuba ya Mkuu wa Wilaya imeonekana kuwavutia wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho kutoka makundi mbalimbali ikiwemo Maafisa Usafirishaji (boda boda) na mama lishe.
0 Comments