Header Ads Widget

SERIKALI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO YA UMEME KWA HARAKA

Na Mwandishi Wetu Chalinze

SERIKALI imeahidi kushughulikia changamoto ya umeme iliyopo nchini kwa kasi ili tatizo hilo iweze kuisha katika kipindi kifupi kuanzia sasa


 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Chalinze wa kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.

Dk Biteko amesema kuwa, katika kipindi cha miezi sita inayokuja ukosefu wa umeme nchini utaisha baada ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kumaliza tatizo hilo nchini. Amesema Watendaji wanafanya kazi ili watanzania wapate umeme wa kutosha.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza TANESCO kupeleka umeme katika shule ya Sekondari ya Moreto ili shule hiyo iunganishwe na umeme mapema. Aidha amechangia kompyuta 10 kwenye shule hiyo maalum kwa matumizi ya TEHAMA kuwasaidia wanafunzi.


Kuhusu Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Biteko ametumia nafasi hiyo kupongeza juhudi zinazofanywa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati na miundombinu muhimu na pia kufanya vizuri katika  makusanyo ya mwaka ambapo wilaya hiyo imekusanya shilingi bilioni 15.

Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa msukumo mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu na fedha hizo zinaelekezwa katika miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi.


Vile vile, Mhe. Dkt. Kikwete amempongeza Mhe. Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini na kumsisitiza awe msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali na kufanya kazi kwa bidii.


Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, madaraja, vituo vya afya ili mkoa huo ukue.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI