Header Ads Widget

WAFANYABIASHARA KASULU WAFUNGUKA UTOAJI RISITI ZA EFD

Mkuu wa wilaya Kasulu Kanali Isack Mwakisu (kushoto) na Meneja wa TRA mkoa Kigoma Deogratius Shuma  (wa pili kushoto) wakibandika kipeperushi chenye ujumbe ikiwa ni   uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wafanyabiashara kutoa risiti wanapofanya mauzo maarufu kwa jina la  TUWAJIBIKE

Meneja wa TRA mkoa Kigoma Deogratius Shuma  (kushoto) akizungumza na wafanyabiashara wa mjini Kasulu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya TUWAJIBIKE  (Katikati) Mkuu wa wilaya Kasulu Isack Mwakisu ambaye alizindua kampeni hiyo

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Wafanyabiashara wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamesema kuwa kitendo cha viongozi na maafisa wa Mamlaka ya mapato (TRA) kuwatembelea kwenye maduka yao kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya mashine za kutoa risiti za kielektroniki kinajenga mahusiano mazuri na kitachochea wafanyabiashara kutumia mashine bila kushikinizwa.


Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyetembelewa na maafisa wa TRA ,Anderson Gobeka alisema kuwa  mpango huo  unajenga kupitia kampeni ya TUWAJIBIKE ni jambo jema na linaimarisha  urafiki baina ya Wafanyabiashara na TRA badala ya ile hatua ya awali ya kufunga maduka na kuwafanya wafabiashara kukimbia kila wanaposikia watumishi wa TRA wanafika maeneo.


Mfanyabiashara mwingine wa Kasulu Nathaniel Sadoki alisema zipo changamoto nyingi zinajitokeza lakini mtindo waliotumia maafisa hao wa TRA na kuzungumza na wafanyajiashara kwa karibu linajenga mahusiano mema na kutatua changamoto hizo kwa mazungumzo.


Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoa Kigoma,Deogratius Shuma amewaongoza watumishi wa mamlaka hiyo kutembea kwenye maduka na kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wa maduka hayo umuhimu wa kutoa risiti za mashine ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato ya serikali.


Shuma aliwaongoza watumishi hao kwenye uzinduzi wa kampeni ya TUWAJIBIKE iliyozinduliwa na Mkuu wa wilaya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu ambapo msisitizo ni wafanyabiashara kutoa risiri za EFD.


Akieleza kuhusu kampeni hiyo Shuma alisema kuwa bado kumekuwa na mwamko mdogo mkoani huo kwa wafanyabiashara kutoa risiti za EFD hivyo kampeni hiyo itaongeza kasi ya matumizi ya mashine lakini pia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.


Akizindua kampeni hiyo Mkuu  wa wilaya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu alisema kuwa utoaji wa risiti ni utaratibu unaowawajibisha watu wote kwa maana ya muuzaji na mununuzi katika kusimamia maslahi ya serikali kuongeza ukusanyaji mapato ambayo yanawezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi wa kawaida.


Mkuu huyo wa wilaya Kasulu alisema kuwa utoaji wa risiti za EFD kwa wafanyabiashara  unawezesha wafanyabiashara hao kulipa kodi stahiki kulingana na biashara waliyoifanya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI