xxxxxxxxxxx
Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yametakiwa kwenda kuisaidia jamii kujiletea maendeleo kwa kupanga mipango yao kutokana na takwimu sahihihi zinazopaswa kufikishwa na wanahabari weledi katika masuala ya takwimu.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ametoa wito huo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari zaidi ya 70 wa mikoa ya Njombe na Ruvuma yaliyoandaliwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS huku akisema endapo wanahabari wataelewa na kwenda kutumia takwimu hizo katika kazi zao itasaidia sana jamii kufahamu changamoto zao na namna ya kukabiliana nazo.
Aidha Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi 2022 Tanzania Bara Bi.Anne Makinda spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema wataendelea kutoa elimu kwenye makundi mbalimbali mpaka vijijini ili wananchi nao waweze kupanga na kutekeleza mambo yao.
Naye Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa anasema wanahabari wanaweza kuisaidia vizuri jamii kujua ni kwa namna gani waweze kufuatilia mahitaji muhimu yanayopaswa kupelekwa kwao kutokana na takwimu kuonesha changamoto zote kila eneo nchini.
Hata hivyo Mtaalamu wa habari na mawasiliano toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Said Ameir amesema mafunzo hayo kwa wanahabari yanapaswa kwenda kusaidia jamii kutekeleza shughuli za maendeleo kwa ushahidi wa kitakwimu.
Kwa upande wao baadhi ya wanahabari kutoka mikoa ya Ruvuma na Njombe Amon Mtega na Lulu Samson wameahidi kwenda kufanyakazi zao kwa weledi mkubwa kwa kutumia takwimu ambazo zitawapa mwanga wananchi kutambua hali ya maendeleo katika maeneo yao.
Sensa ya kwanza ya watu na makazi ilifanyika mwaka 1967 miaka 6 baada ya uhuru na mpaka sasa zimefanyika sensa 6 ikiwa ya mwisho imefanyika mwaka jana 2022.
0 Comments