Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya SOS Children's Village Duniani, Dr. Dereje Wordofa akiangalia maendeleo ya watoto wanaoishi kwenye kituo cha taasisi hiyo kilichpo Ubungo Dar es Salaam |
NA ARODIA PETER_MATUKIO DAIMA App DAR
RAIS wa Taasisi ya Kimataifa ya SOS Children's Village Duniani, Dr. Dereje Wordofa ameiomba Serikali ya Tanzania kutenga bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kusaidia watoto wanaioshi katika mazingira hatarishi na magumu.
Rais Wordofa ameyasema haya juzi Septemba 19, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kumkaribisha nchini iliyoandaliwa na SOS Children's Village Tanzania. Dr. Wordofa pia alitumia nafasi hiyo kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo kupitia vikundi vya vijana na wanawake wanaojihusisha na masuala ya watoto walio kwenye mazingira hatarishi.
Rais huyo wa SOS Duniani ambaye ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania alisema tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ni kubwa zaidi katika nchi masikini ziliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo Tanzania ni miongoni mwake.
Alisema nchi hizo ambazo zinakabiliwa na hali ngumu ya umasikini zina kiwango kikubwa cha watoto wa mitaani ambao wapo kwenye mazingira hatarishi hivyo zinahitajika mbinu mbadala za kisera na kibajeti ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.
Rais huyo aliongeza kusema kuwa SOS Children's Village imesambaa katika nchi 138 Duniani na lengo lake kuu ni kusaidia watoto wasio na wazazi au uangalizi wa kifamilia ili waweze kufikia ndoto zao husani kupata elimu, malazi na mavazi kama walivyo watoto wengine wenye wazazi wao.
"Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada inazofanya kushirikiana na shirika letu kuhakikisha changamoto za watoto zinapata ufumbuzi kupitia sera mbalimbali zinazotungwa na kusimamiwa na serikali kuhusu kumlinda mtoto.
Hata hivyo niombe Serikali ya Tanzania na nchi nyingine za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya watoto wa mitaani na wale walio kwenye mazingira magumu ili waweze kupata elimu, malazi na mavazi na hatimaye wawe na ujuzi wa kusaidia nchi zao." alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa SOS Children's Village Tanzania Bara, Haruna Masebu alisema mifumo iliyowekwa na shirika hilo katika malezi ya watoto kwenye vituo vyao na nje ya vituo umewezesha watoto kupata malezi bora ya kifamilia na hatimaye wengi kupata elimu iliyo bora kupitia ufadhili mbalimbali.
"Mifumo yetu hii imekuwa bora na tumefanikiwa watoto wengi waliopitia kwenye hii mifumo wametunzwa vizuri na wengi wameweza kufika elimu ya vyuo vikuu vilivyopo ndani na nje ya nchi na wengine wameshakuwa watumishi katika sekta mbalimbali, wengine wamekuwa wajasiliamali na haya ndiyo malengo yetu mahsusi.
"Hata hivyo Masebu alizungumzia changamoto mbalimbali wanazikumbana nazo kuwa ni mahitaji yamekuwa makubwa kuliko raslimali zilizopo. Kupitia mkutano huu niiombe Serikali itusaidie kupata wadau zaidi wa kushirikiana nao ili watoto wengi wenye uhitaji waweze kusaidika" alisema Masebu.
Mwenyekiti huyo wa Bodi wa SOS alisema hadi sasa watoto zaidi ya 6000 wamekwishafaidika kupitia SOS Children's Village katika vituo kadhaa vilivyopo mikoa mbalimbali kama vile Mwanza, Arusha na Dar es Salaam.
Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya SOS Children's Village Duniani, Dr. Dereje Wordofa akipanda mti wa kumbukumbu kwenye Kituo cha taasisi hiyo kilichopo Ubungo Dar es Salaam juzi, Septemba 19,2023. |
0 Comments