Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP.
KUKAMILIKA kwa Mwongozo wa Kitaifa wa Elimu kwa Maendeleo Endelevu 2023/2030, ni ishara tosha kwa dunia kuwa Tanzania imejikita katika kutengeneza mazingira ya elimu yatakayochangia kwa kiasi kikubwa katika Maendeleo Endelevu ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Prof. Mkenda Septemba, 22, 2023 jijini Arusha katika hafla ya utiaji saini Mwongozo wa Kitaifa wa Elimu kwa Maendeleo Endelevu 2023/2030, ambapo alisema Tanzania imefanikiwa kufika hatua hiyo, kufuatia makubaliano ya Mawaziri wa Elimu katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Alisema makubaliano hayo ambayo yamepelekea Nchi hizo kufikia makubaliano hasa katika kuidhinisha maandalizi ya Mwongozo wa namna ya kuwa na elimu inayondana na mahitaji ya Maendeleo Endelevu katika nyanja mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.
‘’Tunafurahi kwamba hatimaye sisi tuna mwongozo, na inawezekana ndio nchi ya kwanza ya SADC kukamilisha kazi hii. Tunaishukuru sana UNESCO na UNICEF kwa kazi kubwa waliyoifanya, pamoja Wizara mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar zilizoshiriki katika maandalizi ya mwongozo huo’’ amesema Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda ameeleza kuwa Mwongozo huu una akisi masuala yote yaliyopo kwenye rasimu ya Sera ya elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023, na kwamba elimu ambayo itakuwa inatolewa ya mafunzo ya Amali itawaandaa vijana kikamilifu katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo.
’Ni ahadi kwa watoto wetu na vizazi vijavyo kwamba tumejitolea kuwapa elimu bora zaidi, ambayo inawapa maarifa na maadili yanayohitajika katika ulimwengu unaobadilika haraka huku tukikuza hisia ya uwajibikaji kwa mazingira na jamii’’. Alibainisha Prof. Mkenda
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Salum Abdallah, amesema mwongozo huo umekuja wakati muafaka, wakati Zanzibar ikiendelea kufanya maboresho ya Mitaala Elimu.
‘’kutoka kwenye Mitaala ya maarifa tunaingia kwenye Mitaala ya umahiri ambayo tunaamini kabisa itaweza kumjenga mwanafunzi kutumia maarifa wanayoyapata kwa ajili ya kutatua changamoto zao mbalimbali za kimazingira, kijamii pamoja na kuwapatia maendeleo ya kiuchumi’’ Alisema Abdallah.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Michel Toto ameishukuru Serikali kuendeleza kushirikiana na UNESCO, huku akiwataka Wadau wa Maendeleo kuunga mkono juhudi hizo zinazolenga kutekeleza kwa pamoja mkakati huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
‘’Tunaishukuru serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hapa Tanzania Bara na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kwa nia yake ya dhati kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mwongozo huu wa kimkakati. Mwongozo huu unaakisi matarajio yetu ya pamoja kwenye elimu ya baadaye katika taifa hili'' alisema Toto.
Aidha Toto amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto na (UNICEF) kwa msaada wa Kifedha ambao umesaidia kuratibu maandalizi ya mwongozo huo katika ngazi mbalimbali.
0 Comments