Header Ads Widget

KINANA AZIBEBESHA ZIGO KAMATI ZA SIASA ZA CCM MIKOA..

 


NA WILLIUM PAUL, HAI.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Bara, Abdulrahman Kinana ameagiza kamati za siasa  kila mkoa kumchukulia hatua mwanachama atakayekiuka maadili ndani ya Chama kwa kutaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi kabla ya Muda wa viongozi waliopo madarakani kuisha.


Kinana alisema hayo katika uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022 Jimbo la Hai wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.



Alisema mwanachama anayezunguka kutafuta udiwani na ubunge kabla ya wakati sahihi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa huyo hafai na atakua amepoteza sifa za kuwa mwanachama mwaminifu.


"Nipongeze kamati ya siasa wilaya na mkoa wa Kilimanjaro kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa kwa kasi katika kutatua kero na changamoto mbalimbali za wananchi ikiwemo sekta ya Elimu, Afya na miundombinu, endeleeni kushirikiana na Mbunge wa Hai ili wananchi wapate maendeleo." alisema Kinana.


Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM Jimbo la Hai, Mbunge wa Jimbo hilo Saashisha Mafuwe alisema katika kuhakikisha anaendelea kutatua za wananchi waliompa dhamana kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2020 ni kuwatumikia kwa hali na mali ili kuondoa kero zinazowakabili katika maisha ya kila siku.


Akiainisha baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili Novemba 2020 hadi Oktoba 2022 Saashisha alisema sekta ya Afya ilitengewa zaidi ya Bilioni tatu ambazo zilitumika kukarabati, kujenga zahanati na vituo vya Afya katika maeneo ambayo hayakua na huduma hiyo.

Kwa upande wa Elimu ya awali na msingi ilitengewa zaidi ya bilioni 4 sambamba na miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo korofi lengo likiwa ni kuwaletea wananchi maendeleo.


Pia aliweka wazi mikakati yake ya kutekeleza maendeleo zaidi katika kuboresha soko la kwa Sadala, kiwanda cha kusindika nyama pamoja maziwa ili kuongeza kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


Naye Mkuu wa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro, Amir Mkalipa alishukuru kwa ushirikiano uliopo katika utendaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi aliwasisitiza wanachama kuendelea kudumisha umoja na amani ili Chama kiendelee kuwa na tija kwa wananchi wanaokiamini.

Mwsho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI