Na Mbaruku Yusuph,Matukio Daima APP Tanga.
JESHI la Polisi Mkoani Tanga limefanya msako na kuwatia mbaroni Raia wawili toka Nchini Kenya kwa makosa ya uhalifu wa wizi wa pesa na mali za watu toka katika magari.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi Almachius Mchunguzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema wahalifu hao wamekuwa wakiwavia watu ambao wanatoka Bank kuchukua pesa na kuwafuatilia wanapoegesha magari na kufanya uhalifu huo.
Aidha Kamanda Mchunguzi alisema tukio hilo lilitokea Sep 12 mwaka huu katika maeneo ya barabara ya 13 kata ya ngamiani kati Jijini hapa majira ya saa tano na nusu asubuhi ambapo wahalifu hao walikutwa na Jeshi hilo wakijaribu kutekeleza vitendo hivyo vya kihalifu.
Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao walikuwa wanatumia gari aina ya IST rangi ya silva namba T 931 CVS na baada ya kufanyiwa upekuzi na Jeshi hilo walikutwa na rimoti tatu simu nne tatu za Smarts phone na moja ndogo ya kawaida(kitochi)na vitambulisho mbalimbali ambavyo vilikuwa vinawasaidia kutekeleza uhalifu wao.
Kamanda Mchunguzi alifafanua zaidi na kusema kuwa rimoti hizo zilikuwa na matumizi tofauti ambapo ya rangi nyeusi kwa ajili ya kutolea alam za magari,ya rangi ya kijivu kwa ajili ya kutolea loki za magari na rimoto moja ambayo ni ndogo nyeusi ilikuwa kwa ajili ya kufungulia mageti ya Nyumba.
Alisema baada ya kuhojiwa na Jeshi hilo la polisi walikiri kufanya makosa hayo katika maeneo mbalimbali na moja kati ya makosa waliyoyafanya lilithibitika na kupelekea kufikishwa mahakamani ili waweze kujibu tuhuma wanazokabiliana nazo.
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa hao ambapo ni Idrisa Musa Kasimu miaka 24 fundi umeme na wa pili ni Samweli Kimati Mwenda miaka 35 mfanyabiashara wote ni Raia wa Kenya.
Hata hivyo Kamanda Mchunguzi alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume na taratibu wazisalimishe katika Jeshi hilo au katika Ofisi za Serikali za mitaa na hakuna hatua zitakazochukuliwa kwa mwananchi atakae tii agizo hilo ndani ya muda uliopangwa.
Alisema zoezi hilo la kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume na taratibu limeanza Sept 1 hadi Oct 31 na hatua kali zitachukuliwa kwa mwananchi atakaetiwa mbaroni na Jeshi hilo baada ya muda wa hiari kumalizika.
0 Comments