Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakazi wa kijiji cha Ilininda wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe, wameamua kuchangishana fedha ili kuanza ujenzi na ununuzi wa vifaa vya maabara ya kijiji,itakayosaidia upatikanaji wa vipimo vya magonjwa ya binadamu, ili kuepukana na ramli chonganishi ambazo zimekuwa chanzo cha migogoro, na mauaji.
Kukosekana kwa huduma ya upatikanaji wa vipimo katika ngazi ya vijiji, kunatajwa kuwa chanzo mojawapo cha kukithiri kwa imani za kishirikina ikiwemo ramli chonganishi, kutokana na watu kutumia dawa bila kupima na kubaini aina ya ugonjwa unaomsumbua.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Teodosya Msanga,Ditrick Mlelwa na Exavel Mlelwa mwenyekiti wa kijiji cha Ilininda wamesema adha imekuwa ni kubwa hususani katika upande wa maabara kwani wataalamu wa afya wamekuwa wakibashiri ugonjwa kwa kuwa hakuna vipimo.
Kutokana na changamoto hiyo, wakazi wa kijiji hicho wameamua kushikana mkono na kuchangishana fedha, kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya Akiwemo mwenyekiti wa shirika la kuhamasisha maendeleo kwa wananchi[ECF] bwana Johnson Mgimba ili kuanza rasmi ujenzi wa maabara zoezi ambalo litajumuisha ununuzi wa vifaa.
Changamoto ya Matumizi ya dawa bila vipimo imetajwa kuwa sababu ya kuchochea Ramli chonganishi, kutokana na wakazi hawa kwenda kutafuta chanzo cha magonjwa yanayowasumbua, licha ya kwamba hali imezidi kuwa mbaya kila uchwao.
Lawi Mnyanga ni mkazi wa Ilininda ambaye kwa kushirikiana na wananchi wengine wameiomba serikali kuwashika mkono ili kuongeza nguvu pale watakapoishia ili kukamilisha ujenzi wa maabara na ununuzi wa vifaa tiba.
Kupatikana kwa maabara kwaajili ya huduma za vipimo vya magonjwa ya binadamu katika ngazi ya vijiji kunatajwa kuwa huenda ikawa njia moja wapo ya kupunguza ramli chonganishi katika maeneo hayo sambamba na kupunguza mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
0 Comments