Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na Madarasani zimepelekwa wilayani Makete Mkoani Njombe ili kuondoa changamoto ya mlundikano wa wanafunzi kwa wanafunzi wa kidato cha tano madarasani pamoja na maeneo rafiki ya kulala.
Ripoti ya ujio wa fedha hizo imetolewa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe akiwa katika shule ya sekondari ya wasichana Makete baada ya mkuu wa mkoa wa Njombe kufika kukagua ujenzi wa miundombinu hiyo pamoja na kuzungumza na wanafunzi ambapo amesema katika kipindi cha wiki mbili miundombinu hiyo itakuwa imekamilika.
Awali mkuu wa shule hiyo Sayuni Sanga amesema tayari wanafunzi 87 wa kidato cha tano wamesharipoti shuleni hapo kati ya 454 huku wengine wakiendelea kuwasili.
Aidha mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda amesema licha ya wanafunzi wengi kupangiwa katika shule hiyo lakini watahakikisha wote wanaishi na kusoma vizuri.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Njombe Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Tamasha Lalika,Queen Chengula na Brandina Mwakisole wamesema hatua ya serikali kuwaongezea miundombinu shuleni hapo kunawapa unafuu wa kujisomea kwa uhuru na amani zaidi.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amewasisitiza wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni hapo hadi sasa kufanya haraka kwani shule hiyo imekuwa na kiwango bora kitaaluma ukilinganisha na shule nyingine.
Hata hivyo mkoa wa Njombe ulipata kiasi cha shilingi bilioni 4.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni,Madarasa na vyoo kwenye shule 12 za sekondari hasa zile zinazopokea wanafunzi wa kidato cha Tano katika kipindi hiki.
0 Comments