Header Ads Widget

RC NJOMBE AAGIZA SHULE ZA SEKONDARI ZIFUNGWE CCTV CAMERA.



Na Gabriel Kilamlya - Matukio Daima App, Njombe.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ameagiza shule zote zilizopata fedha za ujenzi wa mabweni kuanza mchakato wa kufungwa kwa camera za CCTV lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi.


Mtaka ametoa agizo hilo mara baada ya kuzulu katika shule ya sekondari Yakobi wakati wa kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano ambapo amesema kutokana na kuwapo kwa historia ya ukiukwaji wa maadili ulioripotiwa shuleni hapo mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe pamoja na maeneo mengine wanapaswa kuchukua hatua za kuwatuma wataalamu wa tehama kwa ajili ya kufunga mifumo ya Camera.


Awali mkuu wa shule ya sekondari Yakobi Mwalimu Editha John amesema tayari wanafunzi wa kike wa kidato cha tano wameshaanza kuripoti kati ya wanafunzi 433 waliopangiwa shuleni hapo.


Afisa elimu mkoa wa Njombe Mwalimu Nelasi Mulungu amesema serikali imeleta shilingi bilioni 4.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwenye shule 12 za sekondari na hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kumsaidia mtoto.


Aidha mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick amesema wakati ujenzi wa mabweni ukitarajia kukamilika katika kipindi cha takribani siku tano tayari wameandaa mazingira mengine ya kuwapokea wanafunzi.


Ahadi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Nancy Abraham,Zacharia Kaduma na Carolina Keneth ni kusoma kwa bidii ili waje kulisaidia taifa katika siku za usoni.


Muhula mpya wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha tano umeanza rasmi sasa huku wanafunzi wakiendelea kuripoti shule.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI