Header Ads Widget

M/KITI UVCCM TAIFA AANZA ZIARA KASKAZINI UNGUJA.


Na Is-Haka Omar-Matukio Daima App, Zanzibar.

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Taifa (MCC) Mohamed Ali Kawaida, amewataka Vijana nchini kuendelea kuamini na kuunga mkono  juhudi zinazofanywa na Serikali zote mbili za Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo inayotoa fursa za kuwakwamua Vijana Kiuchumi.


Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumzia na Vijana, Viongozi na Watendaji wa UVCCM mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa CCM Mkoa huo Mahonda, kwa ajili ya ziara ya kuimarisha uhai wa Chama na Jumuiya hiyo.


Kawaida, alisema Viongozi Wakuu wa Serikali ambao ni Rais Dkt. Samia pamoja na Rais Dk. Mwinyi, wanaendelea kufanya kazi kubwa ya kihistoria ya kutafuta fedha za kuendesha miradi na Sekta mbalimbali za maendeleo ili Wananchi na Vijana kwa ujumla wanufaike.


Katika maelezo yake Ndugu Kawaida, alisema mafanikio yaliyofikiwa nchini yametokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 inayotekelezwa kikamilifu katika maeneo mbalimbali nchini.


Kawaida ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliwasisitiza Vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendelea kushirikiana na Viongozi wa CCM na Serikali kwa ujumla ili wapate nguvu na hamasa za kuwapa vipaumbele vya fursa mbalimbali zinazopatikana katika Mkoa huo.


Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo, alisema UVCCM kwa sasa ina kazi kubwa tatu ambazo ni kuhakikisha uhai wa Jumuiya hiyo unaimarika, Ilani ya CCM inatekelezwa kwa ufanisi unaoendana na mahitaji ya Wananchi wa makundi yote pamoja na kuhakikisha mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia maslahi ya Vijana zinatatua changamoto kwa wakati.


"Vijana wenzangu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,nakupongezeni sana kwa kazi kubwa mnazofanya ndani ya Jumuiya, Chama na Serikali kwa ujumla hivyo nasaha zangu kwenu tuendelee kuwa waadilifu,waaminifu, wabunifu na wachapakazi kwani Viongozi wetu wanafanya kazi kubwa ya kutupigania usiku na mchana ili nasi tunufaike na kujitegemea" alisema Mohamed Kawaida.


Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Ismail Ali Ussi, amesema Vijana wanaendelea kutekeleza majukumu yao vizuri huku wakinufaika na fursa mbalimbali zinazotoka katika ngazi mbalimbali za Serikali na Chama.


"Vijana wa UVCCM katika Mkoa wetu tumefurahi sana na tunakupongeza sana kwani umekuwa ni kiongozi mfano mwenye maono, mchapakazi na mbunifu unayetuwakilisha vizuri na kutupigania kwa nguvu zote popote unaposimama kutuwakilisha",alisema Mwenyekiti huyo.


Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema kupitia utekelezaji wa Ilani CCM imeimarisha Sekta ya Afya kwa kujenga Hospitali za Wilaya mbili katika Vijiji vya Kivunge na Panga tupu huku ikiendelea kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, ili kufikia dhamira ya kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za Afya bila kuzidi Masafa ya kilomita tano.


RC Ayoub, alifafanua kuwa katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa buluu Serikali imetoa jumla ya Boti za kisasa za uvuvi 155,kati ya hizo boti 55 wamepewa  Vijana ili wajiajiri wenyewe.


Kapitia Kikao hicho, RC Ayoub, alifafanua kuwa Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Bandari ya Kisasa katika Kijiji cha Mwangapwani ambapo Vijana wengi wa Mkoa huo watanufaika na ajira sambamba na kufungua milango ya uchumi ya Nchi hiyo kupitia Mkoa huo.


Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo Taifa Mohamed Ali Kawaida, amefuatana na Viongozi mbalimbali wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa, wakiwemo Wajumbe wa NEC, Wabunge na Wawakilishi kutoka UVCCM.


Sambamba na hayo alizindua,kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali zikiwemo Kituo cha Afya Bumbwini Makoba,uwekaji wa jiwe la msingi Soko la Wajasiriamali, uzinduzi wa Maskani ya Vijana Kijiji cha Zingwezingwe, uwekaji wa jiwe la Msingi Skuli ya maandalizi(TUTU) katika Kijiji cha Donge Vijibweni, ukaguzi wa kiwanja Cha Vijana Kijiji cha Kidoti,uzinduzi wa mradi wa Samaki Nungwi na Mkutano wa Hadhara katika eneo la Chaani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI