Na Abdallah Amiri Matukio Daima App Igunga.
Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu Ndaro Kulwa (20) mkazi wa Kijiji cha Imalilo, Kata ya Ngulu wilayani humo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 11 mkazi wa kijiji hicho (jina limehifadhiwa).
Mwendesha Mashtaka wa Serikali upande wa Jamhuri, Grace Lwila aliiambia mahakama mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Lydia Ilunda kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari, 29/2023 majira ya mchana kijijini hapo.
Aliieleza mahakama kuwa katika tarehe hiyo na muda huo mshtakiwa alimbaka mtoto huyo wa miaka 11 na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake.
Mwendesha mashtaka aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu 130 (1) (2) (e) na kifungu 131 (1) sura ya 16 mapitio ya mwaka 2022.
Hata hivyo baada ya kusomewa shtaka mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na ndipo upande wa Jamhuri ulipeleka Mahakamani mashahidi (5) akiwemo mwathirika wa tukio hilo ambao wote walimtambua mshtakiwa.
Baada ya Hakimu kusikiliza ushahidi alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umemuona mshtakiwa Ndaro Kulwa ana hatia.
Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Ilunda alisema kutokana na vitendo vya ubakaji kukithiri maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Igunga, Mahakama inamhukumu mshtakiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.






0 Comments