Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Makundi ya vijana na wanawake mkoani Njombe yametakiwa kuingia kwenye shughuli za uzalishaji kwa vitendo hususani kilimo badala ya kuendelea kunadi kilimo kwenye mitandao ya kijamii ambayo wakati mwingine hakuna uhalisia.
Kauli hiyo inatolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka wakati akifungua mdahalo wa masuala ya kilimo kwa wanawake na vijana chini ya taasisi ya AMDT inayoshughulika na kuwaunganisha wakulima na masoko ambapo ametaka vijana waingine shambani na walime kwa vitendo huku akiwataka kuwa waaminifu kwani kukosekana kwa uaminifu kumekuwa kukiwagharimu wengi.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya AMDT Charles Ogutu amesema taasisi hiyo katika mkoa wa Njombe ina mkakati maalum wa kutoa Mbegu bora za maharage ili kuwainua vijana kupitia sekta ya Kilimo achilia mbali miradi mingine ambayo imekuwa ikiitekeleza.
Afisa Mipango mkoa wa Njombe Bi.Jachinda Chang'a amesema makundi ya wanawake na vijana yamepata mikopo ya shilingi bilioni 1.4,Miche ya Parachichi na Ngano katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na bado jitihada mbalimbali zinaendelea.
Baadhi ya vijana na wanawake akiwemo Joseph Lugome,Eva Luoga na Marietha Putika wamesema bado hawajafanikiwa kupata fursa za mikopo jambo ambalo linawapa wakati mgumu katika kujikwamua kiuchumi.
0 Comments