Header Ads Widget

MRADI WA URAIA WETU WAZINDULIWA KIBAHA.

 

ASASI isiyo ya kiserikali ya YPC ya Wilaya ya Kibaha imezindua mradi wa Uraia Wetu juu ya Utawala wa Kidemokrasia nchini kwa mikoa minne ya Kanda ya Mashariki.


Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi Mtendaji wa YPC Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.


Ilunde alisema kuwa mradi huo ni wa miaka mitatu ambao una lengo la kuendeleza mazingira wezeshi kwa ajili ya ushiriki thabiti wa asasi za kiraia kwenye elimu ya uraia.


"Shughuli kuu zitakazotekelezwa na YPC chini ya mradi wa Uraia Wetu zitajumuisha kuandaa majukwaa ya wakurugenzi wa Asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) kuwezesha majadiliano ya pamoja na serikali,"alisema Ilunde.


Alisema kuwa majadiliano hayo ni ya kufanya uchechemuzi wa masuala ya utawala wa kidemokrasia na maendeleo kwa ujumla pamoja na kuboresha mahusiano na mashirikiano ya kikazi.


"Mradi huu pia unatoa fursa kwa ajili ya kuzijengea uwezo Azaki kujiendesha na kufanikisha shughuli zetu jambo ambalo litawajenga wanufaika wa mradi wananchi na Watanzania kwa ujumla,"alisema Ilunde.


YPC imeingia mkataba huo kati yake na shirika la Foundation for Civil Society (FCS) chini ya udhamini wa Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa ajili ya mradi huo utakaotekelezwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Morogoro.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI