Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru amesema kuwa wananchi watakaoshindwa kujitoa kwa moyo kwa ajili ya kuanzisha miradi ya ujenzi kwenye maeneo yao na kushiriki kwenye utekelezaji wake wanajichelewesha wenyewe na miradi yao haitaweza kutekelezwa haraka.
Kavejuru amesema hayo akihutubia mikutano ya hadhara kwenye vijiji vya Mumbanga na Nyaruboza wilaya ya Buhigwe akijibu malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho wakieleza adha na mateso makubwa wanayopata katika kupata huduma za afya kutokana na kutokuwepo kwa zahanati kijiji hapo na kituo cha afya kwenye kata hiyo.
Mbunge huyo wa Buhigwe amesema kuwa ameshatoa maelekezo kwa uongozi wa kijiji cha Kumbanga na wananchi hao kuanza kukusanya mawe, mchanga na kuanza ujenzi wa boma la zahanati hiyo ili ifike hatua ambayo serikali itamalizia huduma ziweze kuanza lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.
Alisema kuwa hata kwenye ujenzi wa kituo cha afya maelekezo yalitolewa waanze ujenzi na baadaye hela za kupaua na kumalizia zikaja lakini hakuna kilichofanywa na wananchi hivyo pesa zikapelekwa kwenda kukamiliza vituo vya afya maeneo mengine.
Awali wananchi wa kijiji hicho wakitoa malalamiko yao kwa mbunge huyo walisema kuwa wamekuwa wakipata adha kubwa ya kupata huduma za afya na kuwalazimu kutembelea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufuata matibabu mbali na kijiji chao.
Wananchi hao, Cecilia Mpenda na Yohina Isaya kwa niaba ya wananchi wa kijiji wanasema kuwa kwa sasa wanatumia zahanati ya kanisa Anglican iliyopo kijiji hapo Lakini ni changamoto kubwa kwa wajawazito hasa wanaokuwa na changamoto za uzazi ambao hulazimika kutumia kiasi cha shilingi 40,000 hadi 60,000 kufuata huduma za matibabu kwenye kituo cha afya Matyazo wilaya ya Kigoma ambako pia hulazima kulipa kiasi cha shilingi 100,000 hadi 200,000 kwa wajawazito wanaokwenda kujifungua huko.
0 Comments