Makamu wa Raisi Dk.Philip Mpango (wa pili kushoto) akikata utepe kuzindua tawil la Benki ya NMB wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma (kushoto) Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Edwin Mhede
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAKAMU wa Raisi Dk.Philip Mpango amesema kuwa huduma za kibenki vijijini bado ziko hivyo amezitaka benki nchini kupeleka huduma zao kwenye maeneo hayo kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hizo vijijini.
Makamu wa Raisi alisema hayo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma alipokuwa akifungua tawi la benki ya NMB wilayani humo na kusema kuwa bado ni lazima mabenki yafikirie kupeleka huduma vijijini kwenye maeneo yanayokidhi vigezo kwani vijiji vingi kwa sasa vinahitaji uwepo wa huduma za kibenki.
Alisema kuwa yapo maeneo wananchi wanatembea kwa umbali mrefu akitoa mfano wa kijiji cha Kilelema wilayani humo ambao walikuwa wakitembea kilometa 72 na kijiji cha Janda wilaya ya Buhigwe ambao walikuwa wakitembea kilometa 95 kufuata huduma za benki wilayani Kasulu.
Alisema kuwa hali hiyo ilikuwa usumbufu mkubwa kwa wananchi hivyo kusababisha wananchi wengi kuhifadhi fedha zao ndani kwenye mitungi na kwamba pamoja na maendeleo ya kiteknolojia iliyofanya mitandao ya simu kutumika pamoja na mawakala wa benki lakini bado huduma za kibenki bado zipo chinj hivyo zinahitajika sana.
Akielezea kuzinduliwa kwa tawi la NMB wilayani Buhigwe Makamu wa Raisi alisema kuwa lina maana kubwa katika mchakato mzima wa maendeleo ikiwemo kusogezwa karibu kwa huduma karibucna wananchi na kwamba benki hiyo imeleta maendeleo makubwa nchini katika uwekezaji, utekelezaji wa miradi ya
maendeleo,mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya NMB,Edwin Mhede alisema kuwa nia ya kufunguliwa kwa tawi hilo ni kusogeza huduma karibu na wananchi katika wilaya hiyo mpya lakini yenye mahitaji makubwa ya huduma za kibenki kutokana na shughuli za kiuchumi zilizopo.
Awali Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB,Filbert Mponzi alisema kuwa benki hiyo imeweza kufikisha matawi 229 nchi nzima na mashine za kutolea fedha 180 huku ikiwa na mawakala zaidi ya 20,000 na tawi Buhigwe lililofunguliwa linafanya mkoa Kigoma kuwa na matawi sita.
Mponzi ambaye amemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB,Ruth Zaipuna alisema kuwa kufunguliwa kwa tawi hilo kunalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kwa tawi la Buhigwe benki imetenga shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kutoa mikopo na tawi hilo litakuwa na huduma zote za Kibenki kama matawi mengine nchini.
0 Comments