Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mbunge wa jimbo la Buhigwe,Felix Kavejuru amesema kuwa kitendo cha serikali kupunguzwa tozo kwenye biashara mbalimbali kutoka tozo 380 zilizokuwepo hadi kufikia tozo 144 kutachochea baishara kwa wananchi wa mkoa Kigoma na utoa unafuu wa kodi kwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara kwenye vijiji vya Kabwigwa na Mkatanga, Kavejuru alisema kuwa pamoja na kupunguzwa kwa tozo hizo bado Serikali ipo kwenye mipango ya kupunguza tozo nyingine 48 hivyo itatoa nafuu kwa wafanyabiashara lakini kuwawekea mazingira mazuri ya biashara za ndani na zile za kuvuka mpaka kuwezesha biashara kuchangia katika ulipaji kodi kwa hiari.
Alisema kuwa pamoja na kufutwa kwa kodi hizo mkoa Kigoma ambao serikali imeuchagua kuwa mkoa wa kimkakati kibiashara unayo fursa kubwa ya kufanya biashara na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ukanda ambao una watu milioni 56 fursa ya kufanya biashara ikiwa kubwa.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara na wananchi wa jimbo la Buhigwe Mbunge huyo alisema kuwa mkoa huo kwa sasa una miradi mbalimbali inayotekelezwa ambao inalenga kukuza biashara na uchumi wa mkoa ikiwemo mradi wa barabara ya kiwango cha Lami kutoka Manyovu wilaya ya Buhigwe hadi Kabingo wilaya ya Kakonko Kilometa 260 huku Bilioni 23 zikitarajia kutumika kwa ajili ya ujenzi wa forodha ya kisasa kwenye kijiji cha Mnanila Manyovu wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande wao wananchi wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wamesema kuwa kufutwa kwa tozo mbalimbali kulikofanywa na serikali hivi karibuni kutakuwa kichecheo kikubwa cha kuhamasisha wananchi wa wilaya hiyo kupanua biashara kati yyao na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) sambamba na kuzuia magendo.
Kwa upande wake Tumaini Razalo alisema kuwa uwepo wa tozo nyingi kwenye shughuli za biashar ilikuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara na kuwalazimu wengi wao kupita njia za panya na hivyo kuinyima serikali mapato.
0 Comments