Na WMJJWM, Dodoma
Serikali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) imeandaa mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujitegemea watoto waishio katika makao ya watoto nchini kwa kuwafundisha stadi za kazi zitazowawezesha kufanya uzalishaji ili kuondokana na idadi ya vijana tegemezi wanaoishia kujihusisha na vitendo viovu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa utawala kutoka Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali Hassan Mabena, alipotembelea Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo jijini Dodoma Julai 5, 2023 kwa lengo la kukabidhi msaada wa chakula kwa watoto waishio kwenye makao hayo.
Brigedia Jenerali Mabena amesema dhumuni la ujio wao katika makao hayo ya Taifa ya Watoto Kikombo ni kutaka watoto kujengewa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kwenye jamii kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo ili kuondokana na wimbi la watoto na vijana waliojaa mtaani bila kazi yoyote.
"Ujuzi huu watakaoupata watoto na vijana hawa utawafanya kujiamini, kuondokana na makundi yasiyofaa na kuwasaidia kuwa na ufanisi katika katika sekta ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi” alisema Brigedia Jenerali Mabena.
Akitoa maelezo kuhusu kituo hicho Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Tullo Masanja amesema Makao hayo yenye uwezo wa kuhudumia watoto 150, yana eneo kubwa la kuwezesha watoto hao kufanya elimu kwa vitendo ikiwemo eneo la shanba na karakana za ufundi.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wenye lengo la kuwainua na kuwatengenezea mazingira bora watoto waishio kwenye makao mbalimbali nchini.
“Tunashukuru kwa msaada wa chakula ambacho Jeshi la Kujenga Taifa limeuleta kwani chakula ni hitaji la msingi na kila mtoto anahitaji chakula bora kuweza kukua kimwili na kiakili" alisema Masanja.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha kulelea watoto Kikombo, Johnas Tarimo ameshukuru na kupongeza jitihada za Jeshi la Kujenga Taifa kusaidiana na Wizara katika kutoa stadi za kazi kwa watoto waliopo kwenye Makazi hayo kwani itakua chachu wa watoto hao kujifunza zaidi kwa vitendo.
“Watoto hujifunza zaidi kwa kuona uwepo wenu, leo hii ni motisha tosha ya wao kushawishika kuwa kwenye kundi la vijana wenye manufaa na tija kwa taifa hapo baadae kwani hata baadhi yao wameshavutiwa nanyi na pengine wanaweza kutamani kuwa walinzi wa Taifa siku moja" alisema Tarimo.
Jeshi la Kujenga Taifa limekabidhi msaada wa vyakula pamoja na mchele, sukari, mafuta ya kupikia, chumvi na unga wa ugali unaozalishwa na vijana walioko kwenye kambi mbalimbali za JKT nchini.
0 Comments