Uchunguzi uliofanywa na jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera umebaini kuwa chanzo cha moto ulioteketeza bweni katika shule ya msingi na sekondari Istiqaama iliyoko katika manispaa ya Bukoba, ni hitilafu ya umeme.
Akitoa taarifa ya uchunguzi huo kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Kagera Zabron Muhumha amesema kuwa baada ya uchunguzi walibaini kuwa moto ulitoka katika soketi iliyoko kwenye chumba cha matroni, ambayo ilipata hitilafu na kulipuka wakati akichaji simu yake.
“Soketi hiyo ilipolipuka moto uliunguza vitu vilivyokuwa karibu na kusababisha kusambaa kwenye vitu vingine na hatimaye bweni zima kuteketea pamoja na vitu vyote vilivyokuwa ndani ikiwamo magodoro, madaftari, vitabu na sare za shule za wanafunzi” amesema Muhumha.
Ili kukabiliana na matukio ya moto, kamanda huyo wa zimamoto na uokoaji amewataka wamiliki wa nyumba na shule, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mfumo wa umeme, ili kama kuna marekebisho yafanyike haraka kabla ya kusababisha madhara.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shule za Istiqaama Bukoba Farid Said amesema kuwa watagharamia mali zote za wanafunzi zilizoteketea kwa moto.
“Hakuna mzazi hata mmoja atatakiwa kununua vifaa vya mtoto vilivyoungua moto, sisi ni taasisi kubwa tutanunua vifaa hivyo kuanzia magodoro, sare, viatu, madaftari, na tutakarabati jengo lililoungua na kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila wasiwasi” amesema Said.
Julai saba mwaka huu majira ya jioni, bweni la wavulana lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 70 kwa wakati mmoja, la shule ya msingi na sekondari Istiqaama Bukoba liliteketea kwa moto na kusababisha mali zote za wanafunzi zilizokuwa katika bweni hilo kuteketea.
Kwa mujibu wa kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera, hakuna madhara kwa binadamu ikiwamo kifo au majeruhi yaliyotokana na tukio hilo, maana wakati ajali ya moto inatokea wanafunzi wote walikuwa nje wakicheza.
0 Comments