Header Ads Widget

ZITTO KABWE AWAANGUKIA WANANCHI,WANASIASA KIGOMA

 





Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amewaangukia wananchi na wanasiasa wa mkoa Kigoma akiomba radhi kwa mabaya yeyote aliyowafanyia wakati wa mchakato wa harakati za kisiasa na kuwaomba waungane pamoja kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwak 2025.

 

Kabwe alisema hayo katika uwanja wa barafu kwenye mji mdogo wa Mwandiga alipokuwa akimtambulisha aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum CUF, Kiiza Mayeye ambaye amejiunga na ACT Wazalendo.



Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ambaye amewahi kuwa mbunge kwa miaka 15 kwenye majimbo mawili tofauti mkoani Kigoma alisema kuwa wakati wa harakati za kisiasa mambo mengi yanatokea ambayo wakati mwingine yanawakwaza watu ingawa inaweza kuwa bila kukusudia hivyo akachukua nafasi hiyo kuomba radhi na kuomba asamehe kwa yote yaliyotokea.

 


Zitto Kabwe alisema kuwa wananchi na viongozi wa kisiasa mkoani Kigoma wanapaswa kuungana ili kusimamia maslahi ya wananchi kwa pamoja badala ya kutengana kila mmoja kupigania jambo hilo kivyake jambo ambalo linawagombanisha wao kwa wao, alisema kuwa  ili kuikabili CCM wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuifanya ACT kuwa na nguvu ya kusimamia mchakato huo.



Katika mkutano huo Kiongozi huyo wa ACT aliwapokea makada wawili wa CCM akiwemo aliyewahai kuwa Katibu Mwenezi wa CCM mkoa Kigoma Kalembe Masudi ambaye aliwahi pia kuwa diwani wa kata ya Herembe wilaya ya Uvinza sambamba na kumpokea Lumu Mwitu aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM kata ya Mwanga Kusini na Mwenyekiti wa Mtaa.


 

Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo Kiongozi huyo amezungumzia mchakato wa katiba Mpya na kuridhia uendelee ingawa ametaka kuwepo kwa sheria ya uchaguzi ili kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi ambayo Katiba mpya inayopiganiwa iweze kutambua hilo.


Akizungumza katika mkutano huo Mwanachama huyo mpya wa ACT Wazalendo, Kiisa Mayeye alisema kuwa hakukurupuka kama ambavyo amekuwa akishambuliwa kwenye mitandao kwa mpango wake wa kujiunga na chama cha ACT na badala yake alibainisha kuwa alifanya utafiti na kufikia uamuzi huo.

 

Mayeye alisema kuwa alisoma na kuzielewa sera za ACT na namna walivyojipanga hivyo ameona dhamira yake ya kuwapigania wananchi wa mkoa Kigoma itatimia kupitia chama hicho na kwamba usajili unaofanywa na chama cha ACT kwa sasa kitaleta ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 kwenye chama hicho.


Mwanachama huyo mpya wa ACT Wazalendo amempongeza Raisi Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza demokrasia kwa vitendo kwa kuruhusu mikutano ya siasa na kuongeza kuwa kiongozi huyo ataacha kumbukumbu kubwa iwapo atatekeleza na kuumaliza mchakato wa katiba mpya kabla uchaguzi mkuu wa 2025.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI