Na Teddy Kilanga Matukio Daima App Arusha
WAKAZI wa wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wameiomba serikali kupitisha mchakato wa katiba mpya hali ambayo itasaidia kupunguza mgogoro baina ya wananchi na Mamlaka za umma juu ya umiliki wa ardhi.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kumbukizi ya mwaka mmoja ya eneo la Tarafa ya Loliondo na Sale wilayani humo tangu serikali ilipoweka alama za mipaka ardhi ya vijiji 14 na kugeuza kuwa eneo la pori tengefu na baadaye kupandisha hadhi na kuwa pori la akiba la akiba la Poloreti ambapo walisema suluhu ya migogoro ya ardhi ni katiba mpya pekee.
Diwani wa kata ya Nainokanoka,Edward Maura alisema katiba mpya itakuwa suluhu ya migogoro kutokana na utabadilisha mfumo wa uongozi na sherika kandamizi ambazo zinamnyima Mwananchi kumiliki ardhi.
"Kupatikana kwa katiba mpya itasaidia kubainisha na kuweka ardhi vizuri ambapo itatoa umiliki wa ardhi kwa mtu na kutoa hayo mamlaka kwa Rais wa jamuhuri ya Muungano kama inavyofanyika sasa,"alisema Maura nakuongeza kuwa kinachowaumiza wao kama wafugaji ni maeneo ya malisho.
Maura alisema wafugaji mara nyingi huwa hawaendelezi maeneo yao kwani wanaacha kwasababu ya malisho ya mifugo yao hivyo namna pekee ya kuondokana na changamoto ya migogoro ni ujio wa katiba mpya ambayo itasaidia kubadilisha mfumo huo ulipo.
"Ukiangalia baadhi ya nchi jirani kama Kenya ardhi inamilikiwa na wananchi kwa asilimia kubwa hali ambayo inawapa mamlaka katika maeneo yao kwanini sisi tusiige mfano huo,"alisema.
Kwa upande wake diwani wa Viti maalum wa tarafa ya Loliondo,Kijoolu Kakeya alisema kupitia migogoro hiyo ya ardhi kumepelekewa kusitishiwa huduma za afya pamoja na miradi ya maendeleo kwani kwani kwasasa wanatembea umbali zaidi kilometa 30 kufuata huduma hizo.
"Tunaiomba serikali itupatie huduma hizo muhimu kama wananchi wa maeneo mengine kwani sasa hivi vyoo vya wanafunzi mashuleni vimejaa hali wanawake na watoto wanakosa huduma za afya hali ambayo inahatarisha afya za wanafunzi wetu mashuleni,"alisema Diwani Kakeya.
Mwenyekiti wa Viongozi wa mila(Laigwanak) wa wilaya ya Ngorongoro,Metui Oleshaudo alisema hali ya kiuchumi wilayani humo imezolota kutokana na baadhi ya miradi ya maendeleo kusitishwa hivyo wanaiomba serikali wakae meza moja ili kuweza kujenga nyumba moja.
"Kikubwa tunachoomba tukae meza moja na serikali tujadili changamoto na hatma yetu na hata hivyo sisi kama jamii tumeshapeleka maoni yetu na mapendekezo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,"alisema Metui.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro,Mwalimu Raymond Mangwala alisema kwa upande wa elimu serikali imetoa takribani sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule kupitia mradi wa boost ambapo moja ya programu wamejenga vyoo.
0 Comments